CCM yajisifu utekelezaji miradi kwa asilimia 90
Chama cha Mapinduzi CCM, kimesema kimeridhishwa na utekelezaji ya miradi ya maendeleo mkoani wa Arusha kwa zaidi ya asilimia 90.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari amesema chama hicho kimeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka minne wakati wa kutoa tathimini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2015/19.
Polepole, amesema hayo katika kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika mkoani hapo, ambapo amesema chama hicho kimefanya mambo makubwa ndani ya mkoa wa Arusha.
Amesema wakati chama hicho, kikifanya tathimini ya utekelezaji wa Ilani waliangalia zaidi utekelezaji wa miradi maendeleo katika sekta ya afya, maji, elimu, mifugo, kilimo na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Amesema mtaji mkubwa wa chama hicho, kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ni chama kuisimamia serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa vitendo na siyo maneno ya propaganda.
"Kazi ya chama ni kuisimamia serikali, kutoa maoni kwa serikali, kutoa maelekezo kwa serikali na hadi sasa maelekezo hayo yamefanyiwa kazi kwa zaidi ya asilimia 90," amesema Polepole.
Post a Comment