Katambi akomalia madai ya wananchi kwa TAKUKURU, TPA na RAHACO “ Sitokubali Muonewe”
Kufuatia Viongozi wa kata ya Ihumwa kufika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi kudai haki yao ya kutolipwa fedha zao za ardhi wanazoidai Serikali, Kiongozi huyo ameamua kufunga safari hadi eneo hilo na kuzungumza na wananchi hao.
Viongozi wa kata hiyo walifika mapema leo ofisini kwa DC Katambi kumueleza kero zao na ndipo alipoamua kuongozana nao kwenda kuzungumza na wananchi wa Ihumwa na kuwaahidi yeye mwenyewe kulifuatilia jambo hilo hadi watakapopata haki yao.
Akizungumza na wananchi hao DC Katambi amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ina dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake na kwamba fedha ambazo walipaswa kulipwa tayari zilishatolewa na Rais miaka miwili iliyopita.
"Ndugu zangu hilo jambo hata Rais Magufuli akilisikia kwamba bado hamjapata pesa zenu basi sisi viongozi wa chini atatushughulikia, hizi fedha zilishatoka lakini sisi viongozi ndo tunakua wagumu kuharakisha utoaji wake kwa wananchi.
“Sasa nataka niwatoe hofu na niwaahidi kwa dhati ya moyo wangu kwamba jambo hili halihitaji siasa bali maamuzi, sasa mimi kama kiongozi wenu ntalibeba kwa nguvu zote, siwezi kukubali wananchi naowaongoza wateseke kwa sababu ya watu wachache ambao wamekalia hizi fedha ilihali Rais Magufuli alishazitoa kwenu,’ amesema DC Katambi.
Ameongeza kuwa tayari ameshazungumza na Mkuu wa Takukuru ngazi ya Wilaya na Mkoa, RAHACO pamoja na TPA ili kuhakikisha wananchi hao wanapata haki yao na kama ikishindikana basi warudishiwe mashamba yao ili waweze kufanya kilimo.
Post a Comment