Serikali yaonya wanaotelekeza watoto
Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara ametoa onyo wazazi na walezi kutowatelekeza watoto wenye mahitaji maalum wafikishwapo shuleni.
Wito huo umetolewa leo, Bungeni jijini Dodoma na Waitara alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Conchester Rwamlaza aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na serikali juu ya huduma katika shule za watoto wenye mahitaji maalum.
Akifafanua kuhusu suala hilo, Waitara amesema kuwa serikali na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuhakikisha wanawajibika ipasavyo kuwapatia watoto mahitaji muhimu.
"Kwa kweli jambo hili ni jukumu la jamii na sio serikali pekee yake, tukishikamana serikali na jamii jambo hili litakuwa jepesi sana."
Akifafanua baadhi ya changamoto zinazokwamisha katika utoaji wa mgao wa fedha za utoaji huduma katika shule hizo Waziri Waitara amesema kuwa baadhi ya watoto hawawekwi katika mfumo rasmi huku baadhi ya Halmshauri zikishindwa kufikisha taarifa sahihi za mahitaji muhimu ya shule hizo.
"Nitoe wito kwa wabunge, madiwani na viongozi wa vijiji na mitaa tupatiane takwimu sahihi tukipata taarifa sahihi tutapeleka pesa kulingana na uhitaji wa eneo hilo" alisema Waitara
Post a Comment