Mwanafunzi darasa la nne akutwa na mimba ya miezi saba


Mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Welezo halmashauri ya Shinyanga mwenye umri wa miaka 11 amekatisha masomo baada ya kupimwa na kukutwa na ujauzito wa miezi saba. 

Akizungumza katika  kikao cha wenyeviti wa vitongoji 30 vya kata ya Usanda pamoja na wazee wa kimila, ofisa ustawi wa jamii wa halmashauri hiyo, Elizabeth Mweyo amesema mwanafunzi huyo alipewa ujauzito mwaka 2018  na mwanaume ambaye hajafahamika. 

Amesema aliendelea na masomo kama kawaida na baadaye mwalimu wake alimgundua  na baada ya kupimwa alibainika kuwa na ujauzito. 

“Tumekutana hapa lengo kubwa ni kujadili na kupanga mikakati ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni tatizo bado ni kubwa, watoto wanakatisha ndoto zao kama tukio la mwanafunzi wa darasa la nne kukatisha masomo yake,” amesema Mweyo. 

Amesema kuanzia Januari hadi Machi, 2019 wanafunzi 26 wamepata ujauzito na watatu kati ya hao ni wa Shule za Msingi, kuwataka wenyeviti wa vitongoji kuunganisha nguvu kukabiliana na tatizo hilo. 

Akizungumza katika kikao hicho kilichoandaliwa na shirika la Agape linalopinga ndoa na mimba za utotoni,  ofisa mtendaji wa kata ya Usanda, Emmanuel Maduhu amewataka wenyeviti  wa vitongoji kutumia sheria za kimila kuwaadhibu wanaume wanaowapa mimba wanafunzi na kuwaozesha.

No comments

Powered by Blogger.