India imejenga uwezo mkubwa wa TEHAMA Tanzania - Waziri Ndalichako


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema nchi ya India kwa kiasi kikubwa imewajengea uwezo Watanzania wengi kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa viwanda. 

Profesa Ndalichako alisema hayo kupitia taarifa iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa James Mdoe aliyemwakilisha wenye sherehe ya miaka 55 ya Mpango wa India wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Ufundi iliyofanyika katika ubalozi wa nchi hiyo jijini Dar es Salaam. 

Alisema pamoja na India kuiwezesha Tanzania katika maeneo mbalimbali, zaidi wameiwezesha kwenye Tehama kwenye mradi wa kompyuta wa kukusanya takwimu nyingi mara moja na kuzichakata. Alisema ushirikino baina ya nchi hizo mbili ulianza muda mrefu tangu mwaka 1974 ambapo watu mbalimbali wamepata udhamini kwa ajili ya kujifunza teknolojia na masomo mbalimbali. 

"Mwaka huo 1974, India ilianza kutoa udhamini kwa watu 24 lakini hivi sasa wamefikia 500 wanaokwenda kila mwaka,” alisema Profesa Ndalichako. Naye Balozi wa India nchini, Sandeep Arya alisema ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili umewezesha miradi mikubwa ya India ambayo inaendelea ikiwemo ule wa usambazaji maji kutoka Ziwa Victoria hadi Tabora, Nzega, Igunga na vijiji 89 ambavyo vinapitiwa na mradi huo kwa thamani ya Sh bilioni 600. 

"Miradi mingine miwili ya usambazaji maji katika jiji la Dar es Salaam, Chalinze na Zanzibar nayo pia inaendelea. Tumetoa ahadi zaidi ya shilingi trilioni 1.15 zitatolewa kwa ajili ya usambazaji maji katika miji mingine 26," alisema.

No comments

Powered by Blogger.