Serikali ya Awamu ya Tano inawajali wafanyabiashara wadogo - DC Muro


Wajasiliamali maarufu kama Wamachinga Wilayani Arumeru, wamemiminika kugombea vitambulisho vya ujasiliamali wakati Mkuu wa Wilaya hiyo, Jerry Muro, akizindua rasmi zoezi la utoaji wa vitambulisho hivi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo. 

Uzinduzi wa ugawaji vitambulisho hivyo umefanyika katika Halmashauri ya Arusha DC  eneo la Ngaramtoni na Halmashauri ya Meru katika eneo la Uwanja wa  Ngaresero na kuhudhuriwa na mamia ya wafanyabiashara ndogondogo ambao watanufaika na zoezi hilo. 

Wilaya ya Arumeru inayoongozwa na Jerry Muro ina Halamashuri mbili za Arusha DC na Arumeru ambapo kwa kuanzia, Wilaya hiyo itatoa zaidi ya vitambulisho elfu sita kwa wafanyabiashara ndogondogo humo. 

Mkuu wa Wilaya aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwainua kiuchumi na kuwaondolea adha ya kubugudhiwa mara kwa mara na ndio maana Rais Magufuli aliamua kuwatengenezea vitambulisho hivyo ili waweze kutambulika rasmi na kufanya biashara zao bila usumbufu. 

“Serikali ya Awamu ya Tano inawajali wafanyabiashara wadogo kama nyinyi na ndio maana Mheshimiwa Rais kaweka utaratibu wa kuwapatia vitambulisho na mimi Mkuu wenu wa Wilaya nitahakikisha wajasiliamali ambao mauzo yenu hayazidi milioni nne kwa mwaka mnapata vitambulisho hivi”, alisisitiza Muro. 

Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilayani Arumeru, Musa Sudi, alisema kuwa TRA itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waweze kutambua fursa zilizopo za kufanya biashara kupitia vitambulisho vya “Magufuli” hatua ambayo itawarahisishia ulipaji wa kodi pamoja na kuwasaidia kukua kibiashara. 

No comments

Powered by Blogger.