Sitaki kuwa kama Mourinho - Xavi

 Mchezaji wa zamani wa klabu ya Barcelona, Xavi Hernandez amesema kuwa hawezi kutumia staili ya kocha Jose Mourinho kufundisha timu zake atakapokuwa kocha licha ya kuvutiwa na mafanikio yake. 

Amesema hayo ikiwa imebakia siku moja kabla ya klabu yake ya zamani ya Barcelona kukutana na Inter Milan katika mchezo wa klabu bingwa Ulaya Jumatano hii, ambapo ameelezea uzoefu wake alipocheza na Inter Milan ya kocha huyo msimu wa 2010/11. 

Akiuzungumzia kumbukumbu ya mchezo huo pamoja na staili ya ufundishaji ya Jose Mourinho, Xavi amesema, "hiyo ndiyo staili yake, ameitumia akiwa na Chelsea na Real Madrid, anazipa umakini kila taarifa, anafunga kila nafasi na kuhakikisha hupati mwanya wowote". 

"Ninapenda aina tofauti tofauti za kandanda, simaanishi kumkosoa lakini sifurahii kucheza mpira wa aina yake na timu zangu zote hazitocheza namna hiyo", ameongeza. 

Xavi ambaye anatimiza miaka 39 mwezi Januari mwakani, anacheza katika klabu ya Al Sadd SC ya nchini Qatar baada ya kuondoka Barcelona msimu wa 2015/16, akiwa ameichezea michezo 505 na kufunga mabao 58 tangu mwaka 1998. 

Mkongwe huyo amethibitisha kuwa huu ndiyo msimu wake wa mwisho kucheza soka, baada ya kustaafu anatarajia kugeukia kazi ya ukocha. 

No comments

Powered by Blogger.