Zijue kazi zinazosababisha maumivu ya uti wa mgongo


Wafanyakazi wengi katika maeneo yao ya kazi huweza kujikuta wanatumia muda mwingi kukaa. Wasafiri nao hujikuta wakipanda mabasi na kukaa pia kwenye kiti. Mazingira ya viti wanavyokalia mara nyingi huweza kuwa ni tatizo kwao. 

Vilevile kazi wanazofanya zinatofautiana ikiwamo wapo wanaotumia muda mwingi kuinama, kukaa au kusimama. Makundi yote haya yanaweza kuwa katika hatari ya kupata matatizo ya mgongo endapo watafanya kwa muda mrefu. 

Wapo ambao muda mwingi kazi zao ni kusafiri na huku akitumia muda mwingi kukaa katika kiti cha gari kwa muda mrefu. Barabara zinazohatarisha matatizo ya uti wa mgongo ni zile zilizo na lami yenye matuta na zisizo na lami zenye mashimo. 

Matukio haya kwa wafanyakazi na wasafiri yanaweza kutupa picha na hali juu ya hali zetu za kiafya na kazi tunazofanya au aina ya vyombo tunavyosafiria. 

Pamoja na hali hiyo matatizo ya mgongo yanaweza kutokana na umri kuwa mkubwa, kutokuwa na muda wa mazoezi kutokana na kazi na kujifungua. 

Maumivu ya mgongo ni moja ya matatizo ya kiafya yanayojitokeza mara kwa mara na huathiri zaidi misuli na mifupa ya mgongo. Tatizo hili linawaathiri karibu asilimia 40 katika moja ya hatua za maisha yao. 

Maumivu ya mgongo yapo ya kawaida; chini ya wiki 6, yapo ya kati; wiki 6 hadi 12 na maumivu sugu; ambayo yanadumu kwa zaidi ya wiki 12. Maumivu haya yakianishwa zaidi yanaweza kutokana na kupata majeraha ya kawaida au mambo yasiyo ya majeraha na chanzo maumivu hayo kinaweza kuwa eneo husika au maumivu yalitokea mahali pengine mwilini. 

Mara nyingi maumivu haya chanzo na sababu hasa hakigunduliki moja kwa moja na hakujitokezi mapema, lakini inaaminika kuwa chanzo cha maumivu haya huenda yametokana na kujeruhiwa kwa misuli au mifupa ya mgongo. 

Endapo itatokea maumivu hayo kutoisha baada ya matibabu ya kawaida ama kuambatana na viashiria hatari kama vile kupungua uzito kusikokuwa na sababu maalumu, homa kali, kushindwa kuhisi chochote maeneo ya makalio au miguu na kushindwa kujongea vizuri, hali kama hizi lazima hatua za haraka zitahitajika kwa ajili ya uchunguzi kwani ni kawaida maumivu ya mgongo kupotea baada ya matibabu chini ya wiki sita kwa asilimia 40-90 ya wagonjwa. 

Umbile la mgongo ni kama vile herufi S likiwa na maeneo makuu manne, yaani cervical, thoracic, lumber, sacral na coxgeal. Mgongo unaundwa na pingili za vifupa 24 vilishikizwa na kutengeneza maungio. Pia kuna vifupa tisa vilivyoshikamana katika muishilio wake. Hivi ndivyo vinaonekana kama mkia na kufanya jumla ya mifupa 33. Katikati ya pingili hizi huwa na kitu kama santuri inayofanana na plastiki, pia huwa na matundu ya pembeni na kati, na kutengeneza mfereji maalumu unaopita uti wa mgongo. 

Uti wa mgongo ndiyo chanzo cha maelfu ya mishipa ya fahamu inayopeleka na kuleta taarifa za mfumo kutoka sehemu mbalimbali mwilini na kuzipeleka katika ubongo kwa ajili ya tafsiri. Kifupa cha kwanza na cha pili ndivyo vinavyoweza kufanya mijongeo mbalimbali kama vile inayoashiria ndio na hapana kwa mwitiko wa kichwa. Vilevile mifupa 12 ya mbavu hukutana na pingili za mifupa ya mgongo na kutengeneza ungio. 

Kazi kuu ya mgongo ni kuuwezesha mwili kuwa na umbile maalumu linalowezesha mwili kusimama, kazi ya kuulinda uti wa mgongo ambao ni rahisi kudhurika na kiuunganishi cha kichwa na kiwiliwili. Vilevile mwishilio wa mgongo ndio kwa kiasi kikubwa unasaidia kutembea. Maumivu ya mgongo hujitokeza zaidi kwa watu wa umri wa miaka 20 hadi 40. Baadaye nusu ya wagonjwa hupata maumivu makali kuliko ilivyokuwa mwanzoni. 

Pale inapotokea maumivu yakawa sugu huambatana na matatizo mengine kama vile kukosa usingizi, kuhisi kulala mara kwa mara lakini usingizi huwa mfupi. Hii ni kutokana na kushtuka mara kwa mara nyakati za usiku. Katika hatua za baadaye tatizo hili husababisha matatizo ya akili kama vile msongo wa mawazo, sinona na woga uliopitiliza. 

Inaaminika ni matokeo yaliyotokana na majeraha ya kawaida ya misuli na mifupa, ikiwamo kazi tunazozifanya katika maeneo yetu ya kazi na mienendo na mitindo ya kimaisha ikiwamo kutofanya mazoezi ya mwili. 

Vilevile uzito uliokithiri, uvutaji tumbaku, kuongezeka uzito kipindi cha ujauzito, shinikizo la kimwili, kutofanya kazi, mkao wa ovyo na ulalaji usioendana. Haya ni miongoni mwa mambo yanaambatana na maumivu ya mara kwa mara ya mgongo. Kwa upande wa magonjwa ya mwili ni pamoja na baridi yabisi ya mifupa, shambulizi la maungio, kunywea na kuchoropoka kwa santuri za mgongo. 

Mengine ni santuri za mgongo kujipenyeza katika uti wa mgongo, kuvunjika kwa vifupa vya mgongo, mfano kumomonyoka kwa vifupa. Yapo mambo mengine yanayosabisha ingawa ni nadra sana ni saratani au uvimbe au uambukizi ikiwamo TB ya mgongo. Tatizo hili kwa kinamama huambatana na maumivu ya mgongo kama vile kujipandikiza kusiko kawaida kwa tishu za mfuko wa uzazi, saratani ya mirija ya uzazi, ovari na uvimbe wa mfuko wa uzazi. 

Karibu nusu ya wanawake waliowahi kuwa wajawazito hupata tatizo la maumivu ya chini ya kiuno wakati wa ujauzito. Hii ni kutokana na mabadiliko ya ujauzito yanayosababisha kuwa na mkao usio wa kawaida na mgandamizo wa misuli na nyuzi zinazoshika mifupa ya kiuno na mgongo. Ajali zilizoambatana na umri mkubwa au matumizi ya muda mrefu ya dawa jamii ya corticosteroidi huashiria kuvunjika kwa pingili za mifupa ya mgongo. Kuwa na maumivu makali sana ya chini ya mgongo kwa mtu aliyewahi kufanyiwa upasuaji mwaka uliopita. 

Uwapo wa homa kali, uambukizi njia ya mkojo, upungufu wa kinga mwilini, utumiaji wa dawa kwa njia ya mshipa, ni viashiria vya uwepo wa maumbukizi mwilini. Mambo haya ni viashiria hatari kuwa mwilini kuna tatizo kubwa hivyo hatua za haraka zinahitajika.

No comments

Powered by Blogger.