Madharaya utumiaji wa sukari kwa wingi
WENGI wetu tumeshasikia ushauri wa kula sukari kidogo – ushauri ambao ni mzuri kiafya. Lakini licha ya tahadhari mbalimbali zinazotolewa na wataalamu wa afya kuhusu madhara yatokanayo na ulaji mwingi wa sukari, bado idadi kubwa ya watu hupenda kutumia sukari kwa wingi kwa njia mbalimbali.
Utumiaji wa sukari siyo lazima ile sukari nyeupe (white) au kahawia (brown) pekee, bali pia hata sukari asilia inayopatikana kwenye matunda, maziwa, asali, vinywaji baridi, pombe, baadhi ya nafaka, n.k. Hizo zote ni aina za sukari ambazo zinatofautiana faida na madhara.
Wakati viwanda vya uzalishaji sukari duniani vinaongezeka, tatizo la unene kupita kiasi kwa binadamu nalo linaendelea kuongezeka. Sukari inahusika kwa kiasi kikubwa na tatizo la kuongezeka kwa unene wa kupindukia (obesity). Kwa watu wanene, ulaji wa sukari hata kijiko kimoja tu kwa siku, huchangia kwenye tatizo. Sukari ni ya kuepukwa, siyo tu kwa watu wanene, bali hata kwa watu wengine wenye kujali afya zao.
- Sukari huweza kuathiri ukuaji wa homoni mwilini (kitu ambacho ni muhimu kwa kumfanya mtu kuishi na afya njema wakati wote).
- Sukari ndiyo chakula cha saratani mwilini
Sukari huongeza lehemu mwilini (cholesterol)
- Sukari huweza kusababisha kizunguzungu na kudhoofisha mwili kwa watoto
- Sukari huweza kudhoofisha nguvu ya macho
- Sukari huweza kuzuia utembeaji wa protini mwilini
- Sukari huweza kusababisha mzio wa chakula (food allergies)
- Sukari huchangia ugonjwa wa kisukari
- Sukari huweza kusababisha ugonjwa wa moyo
- Sukari huweza kuharibu umbo la vinasaba vya mwili (DNA)
- Sukari huweza kusababisha utukutu, utundu na kukosa umakini kwa watoto
- Sukari huweza kuchangia kupunguza kinga ya mwili dhidi ya magonjwa yatokanayo na wadudu aina ya bakteria (infectious diseases).
Hizo ni baadhi tu ya hizo sababu 146. Je, kwa kujua sababu zote zilizothibitishwa kuhusu madhara yatokanayo na sukari, kuna sababu gani ya kuendelea kupenda kutumia sukari? Kitu kizuri pekee kuhusu sukari ni kwamba kina ladha tamu na tunapokula, tunajisikia raha. Hapa ndipo pahali panahitaji kuangaliwa kwa makini.
Kiasilia, mwanadamu ana ladha sita tofauti, zikiwemo za uchungu, utamu, ukali, ukakasi. Hivyo kuacha kabisa ulaji wa ladha tamu kunaweza kusababisha madhara mengine ya kibaiolojia na ndiyo maana watu wengi hushindwa kujizuia kutumia sukari, hasa kwa watoto ambao kwao huonekana ni jambo lisilowezekana kabisa kuacha kulamba sukari.
Hata hivyo, kuna habari njema kuwa unaweza kutumia mbadala wa sukari na kupata ladha ya utamu katika vinywaji au vyakula vyako bila kuwa na madhara. Moja ya mbadala wa sukari anayeaminika na wengi tangu enzi na enzi, ni asali, ambayo unaweza kuitumia kwenye vinywaji mbalimbali bila kuwa na madhara.
Hata hivyo, baadahi ya wataalamu wanasema kuwa kwa kuwa asali nayo ina 'fructose', huenda ikawa na mdhara pia, ingawa kwenye vitabu vya dini na baadhi ya wanasayansi wameielezea asali kama kitu kisicho na madhara mwilini licha yakuwa nayo ni tamu kama sukari.
Baadahi ya wanasayansi wamependekeza zaidi mbadala wa sukari kuwa ni 'Stevia' na 'Xylitol', ambavyo vinatokana na mimea na majani lakini vina ladha ya utamu kuliko hata sukari. 'Stevia' na 'Xylitol' hutumika zaidi katika nchi za Ulaya, Japan na Amerika ya Kusini, kwetu Afrika hazijulikani sana na sidhani kama zipo.
Jambo la msingi ni kujua kwamba sukari tunaipenda, lakini siyo chakula kizuri kama tunavyoweza kudhani, hivyo tujitahidi kuiepuka kadri tunavyoweza kwa kutumia mbadala kama asali, pale tunaposhindwa kabisa kuiepuka, basi tutumie kwa uchache sana.
Post a Comment