Klabu ya Simba yakanusha taarifa ya kumfukuza mchezaji wao

Klabu ya Simba imekanusha taarifa za kumfukuza mchezaji wake Yusuph Mlipili kama ambavyo imekuwa ikielezwa badala yake mchezaji huyo yupo kambini na wenzake wakijiandaa na michezo mbalimbali ya ligi. 

Akiongea leo jijini Dar es salaam msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara amesema anashangaa taarifa za kufukuzwa kambini kwa Mlipili zimetoka wapi wakati mchezaji huyo yupo kambini na hana tatizo na klabu. 

''Timu yetu imesafiri leo kuelekea Tanga kwaajili ya mchezo wetu dhidi ya JKT Tanzania na nimeongea na daktari wa timu kanihakikishia kuwa wachezaji wote wapo salama isipokuwa Asante Kwasi ambaye ni majeruhi lakini nashangaa kuna taarifa za Mlipili kufukuzwa kambini sijui wamezito wapi'', amesema. 

Mbali na hilo Manara amesema maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa klabu hiyo na ule wa Uchaguzi yamekamilika na kuwataka wanachama kujitokeza kwa wingi siku Jumapili 4/11/2018. 

Manara amesema kujitokeza kwa wingi kwa wanachama ndio kutasaidia kuchagua Mwenyekiti wa klabu na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wenye sifa na wanaokubalika na klabu.

"Simba ya sasa inahitaji viongozi ambao wataifanya Simba licha ya kujiendesha kiuchumi lakini iweze kupigania makombe yenye hadhi ikiwepo klabu bingwa Afrika.Wawe watu wenye mipango ya kuipeleka Simba mbele, lazima tuliangalie hilo'', amesema.

No comments

Powered by Blogger.