UNICEF: Zaidi ya watoto 2000 wanahitaji msaada

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto la UNICEF limeonya kuwa takriban watoto 2,300 walio katika msafara wa maandamano ya watu ambao sasa uko kusini mwa Mexico wanahitaji ulinzi na huduma muhimu kama vile afya, maji safi na huduma za kujisafi. 

Msemaji wa UNICEF Marixie Mercado akizungumza na waandishi habari mjini Geneva Uswisi leo amesema watoto hao wako kwenye safari hiyo ndefu na ngumu na kwamba .. 

“Watoto  hao wanakabiliwa na hali mbaya ya hali ya  hewa pamoja na hali ya  joto kuwa kali huku kukiwa hakuna mahali pazuri pa kupumzikia..Baadhi wameugua  na wengine wameishiwa maji mwilini kwa mujibu wa kikosi cha UNICEF kilichoko huko.” 

Amesema UNICEF  na washirika wake  Mexico wanapatia watoto na familia vifaa vya muhimu kama vile  maji ya kunywa lita zaidi ya 20,000, sabuni, pedi na dawa ya chumvi  ya kuzuia kupungukiwa na maji mwilini. 

UNICEF imesema idadi kubwa ya watoto na familia katika msafara huo wanakimbia ukatili wa kijinsia, upokonywaji wa mali kinguvu, umaskini na fursa finyu ya elimu bora na huduma za kijamii katika nchi za El Salvador, Guatemala na Honduras. 

“Kwa bahati mbaya, mazingira hayo ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa mamilioni ya watoto kwenye ukanda huo. Kila siku familia inakabiliwa na mazingira haya magumu na kufanya uamuzi mgumu wa kuacha nyumba zao, jamii, nchi ili kusaka usalama na maisha bora kwingineko,” imesema UNICEF. 

UNICEF imeongeza kwamba huku walioko katika msafara huo  wakiwa wanahisi kuwa salama yao ni kutembea katika makundi makubwa, kuliko  njia za vichochoroni, hali hiyo inaleta wasiwasi hususan kwa watoto. 

UNICEF inasema safari yenyewe ingawa kuwa ni mbali na ndefu, lakini pia ni ya hatari mno kutokana na uwezekano wa kuhadaiwa, kufanyiwa ukatili na pia  kunyanyaswa. 

UNICEF imekariri wito wake wa kila mara kwa serikali kuweka mikakati bora kwa watoto katika sheria zao za uhamiaji ili kuweka familia pamoja  na pia vituo mbadala vya  uhamiaji ambapo watawaweka watoto hao.

No comments

Powered by Blogger.