Simba na Yanga zatumia Milioni 11 Moro
Kikosi cha timu ya Yanga.
IMEBAINIKA kuwa, timu za Simba na Yanga, zote zimetumia zaidi ya Sh11 milioni kwa ajili ya kambi zao mkoani Morogoro zilipokuwa zikijiandaa na mchezo wao wa leo Jumapili wa Ligi Kuu Bara. Simba ambayo iliingia Morogoro Jumapili ya wiki iliyopita na kuondoka Alhamisi ya wiki hii, ilifikia kwenye Hoteli ya Moro View iliyopo maeneo ya Nanenane.
Yanga ambayo nayo iliingia Morogoro Jumatatu ya wiki hii, iliondoka juzi Ijumaa huku ikiweka makazi yake kwenye Hoteli ya Kingsway iliyopo mitaa ya Msamvu. Simba ambayo ilikuwa na msafara wa watu wasiopungua 29. Kulala Moro View Hotel mtu mmoja Sh25,000 watu 29 ni Sh 725,000, kwa siku nne walizolala hapo ni sawa na Sh 2,900,000 kwa watu hao wote.
Sehemu ya kufanyia mazoezi, Jumatatu Simba ilifanyia kwenye Uwanja wa Highland uliopo Bigwa ambapo gharama zake si chini ya Sh 150,000 kwa siku. Siku ya Jumanne, Jumatano na Alhamisi, Simba ilifanyia kwenye Uwanja wa Jamhuri ambapo kwa mujibu wa wasimamizi wa uwanja huo, timu ya ligi kuu kama Simba, kwa siku moja inawapasa kulipia Sh 100,000 ambapo asubuhi ni Sh 50,000 na jioni 50,000.
Kikosi cha timu ya Simba
Simba ilikuwa ikifanya mazoezi uwanjani hapo jioni pekee kasoro Alhamisi ilifanya asubuhi. Kwa siku tatu ni sawa na Sh 150,000. Jumla Simba imetumia si chini ya Sh 3,200,000 ikiwa ni gharama za mazoezi na malazi pekee.
Kwa upande wa Yanga ambayo yenyewe ilikuwa na msafara wa watu si chini ya 30, hoteli waliyofikia mtu mmoja kulala ni kuanzia Shilingi 70,000 mpaka 100,000. Kwa hesabu za harakaharaka, kwa usiku mmoja wametumia shilingi 2,100,000. Kwa siku nne ni Sh 8,100,000.
Kikosi cha timu hiyo kilikuwa kikifanyia mazoezi kwenye Uwanja wa Highland ambao gharama yake haipungui shilingi 150,000. Kwa siku nne ni shilingi 600,000. Ukijumlisha gharama hizo za malazi na uwanja wa mazoezi, unapata shilingi 8,700,000. Ukichukua gharama za Simba na Yanga walizozitumia wakiwa Morogoro kwa malazi na mazoezi, unapata shilingi 11,900,000.
Post a Comment