Jambo muhimu unalopaswa kujifunza kwenye mahusiano

Mungu ni mwema ametujalia pumzi, hakika tumshukuru. Kwa wale wenye changamoto mbalimbali basi niwape pole na ninaombea ziishe haraka inshallah!  Kama ilivyo ada, kila wiki huwa nakuja hapa nikiwa na mada mpya. Wiki hii kama inavyojieleza hapo juu, nimekuiwa nikipata meseji nyingi sana kutoka kwa wasomaji wangu wakilalamika kuteswa kwenye mahusiano yao.

Wanalalamika kwamba wanatamani kuwa na watu sahihi lakini kila uchwao wanaambulia maumivu. Wanapoteza imani na matumaini tena. Inafika mahali wanaamini kwamba, ndoa wameumbiwa wengine na wao watabaki kuwa hivyo walivyo miaka nenda rudi.

Tujifunze
Ndugu zangu, tunapaswa kutambua kwamba maisha ya uhusiano yana siri kubwa sana. Kwa wale ambao bado hawajaingia kwenye uhusiano sasa, hawana uhakika wa moja kwa moja kwamba wapenzi walionao sasa hivi wanaweza kuingia nao kwenye ndoa au la. Yaani naweza kusema ni kama vile mchezo wa kamari. Unakutana na mtu humjui, ujenge imani naye na mwisho wa siku mfikie maamuzi ya kufunga ndoa. Hapa katikati hapa lazima mtapitia sarakasi nyingi, lazima akili yako ijiweke tayari kwa hilo.

Changamoto ambayo inawakumba wengi ni kwamba, hawajiandai kisaikolojia katika hili hivyo kujikuta kwenye maumivu makali. Tunawaamini wenza wetu kwa haraka, tunatupa akili na mawazo yetu haraka kwao mwisho wa siku unakuja kuambulia maumivu.

Nini cha kufanya?
Unachotakiwa kufanya, kabla hujamkabidhi mtu moyo wako wote unapaswa kujiandaa kisaikolojia kujua kwamba yule ni binadamu kama walivyo binadamu wengine. Anaweza kuwa tapeli, anaweza kuwa muongo na anaweza kuwa mhuni au hata jambazi.

Anaweza kuwa katili, anaweza kuwa na hofu ya Mungu anaweza kuwa hata muuaji. Hivyo unapaswa kujiweka tayari katika hilo. Akili yako iwe na uwezo mpana wa kung’amua mambo kabla ya kufanya maamuzi. Sio unakutana na mtu leo, unamkabidhi moyo wako na kuona anafaa, utaumia bure. Jipe muda fulani wa  kutafakari. Jipe muda mzuri wa kumsoma mwenzako ni mtu wa aina gani kabla ya kufanya maamuzi sahihi.

Mkatae ambaye si sahihi
Wala akili yako isiumie eti kwamba umekuwa ukikutana na wengi na wote umeachana nao na sijui umri unaenda, bora uchelewe kuingia lakini uingie na mtu ambaye ni sahihi. Unachotakiwa kujua ni kwamba, hakuna mtu ambaye ameingia kwenye ndoa bila kukumbana na changamoto. Kama wapo basi ni wachache.

Zikubali changamoto
Unatakiwa kukubaliana na changamoto za matapeli. Kikubwa unachotakiwa ni kutouchosha moyo wako kwa kupenda watu ambao si sahihi. Kabla ya kumkabidhi moyo wako, jiridhishe kwanza kwamba huyo mtu ni mtu wa aina gani? Lazima umsome kwamba ana ubinadamu? Ana hofu ya Mungu? Historia yake kwa maana ya familia je ni njema? Kuna vitu unaweza kumbadilisha lakini lazima ujue kupima kwamba jambo au tabia fulani aliyonayo mwenzako unaweza kumbadilisha?

Kama huwezi ni vyema ukamuacha akabaki tu kuwa kama rafiki na umueleze ukweli kwamba hamuendani, mbaki kuwa marafiki wa kawaida na maisha yaendelee. Hakuna sababu ya kuwa na mtu ambaye unaona kabisa kaa la moto liko usoni.

Mpe muda
Mweke karibu, msome kama unaweza kwenda naye na ukiona huwezi basi mueleze tu abaki kuwa rafiki wa kawaida. Mueleze kwamba ili muweze kuendana na kuishi kwa amani na upendo, mnapaswa kufanana kitabia vinginevyo mtakaribisha maafa huko mbeleni.

No comments

Powered by Blogger.