58,904 kufikishiwa elimu ya sheria Nanyumbu
Katika kuhakikisha jamii inatambua haki na wajibu wake walau kwa uchache. Shirika la Ushauri na Mafanikio kwa Jamii(CHPO) ambalo linatoa msaada wa kisheria katika wilaya ya Nanyumbu, mkoa wa Mtwara limelenga kufikisha elimu ya sheria wilayani humo kwa watu 58,904 hadi kufikia mwezi Septemba,mwaka 2020.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa kituo hicho, Dikson Mwichaha, jana alipozungumza na Muungwana Blog mjini Mangaka.
Mwichaha alisema wamebaini kwamba elimu bado inahitajika wilayani humo. Kwani watu wengi, hasa wanawake hawazijui haki zao. Kwahiyo wamekuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kinjisia.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo wamekusudia kufikisha elimu ya sheria inayohusu mambo yanayosababisha migogoro na ukatili wa kijinsia. Ambapo hadi kufikia mwezi Septemba,mwaka 2020 wawe wamefikisha elimu hiyo kwa watu hao 58,904.
" Tumepanga kujikita zaidi katika maeneo ya ndoa na talaka, mirathi, ardhi na matunzo ya watoto. Tumebaini kwamba hata migogoro mingi inayohusu matunzo ya watoto inatokana na uvunjwaji ndoa kiholela. Kibaya zaidi akinamama wanaachiwa jukumu la kutunza watoto. Huku wanaume wakienda kuoa wanawawake wengine. Matokeo yake ni kuongezeka watoto wa mitaani na mimba za utotoni,'' alisema Mwichaha.
Mratibu huyo alibainisha kwamba hadi mwezi huo wa Septemba 2020 wanatarajia kutoa msaada wa kisheria kwa watu 375. Huku akiwa na matumaini makubwa kwamba wanaweza kufikisha elimu kwa idadi hiyo ya watu. Kwani kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka huu pekee wameweza kufikisha elimu kwa watu 12,500.
Mwichaha aliutaja mkakati wakwanza ili kufanikiwa azima hiyo ni kufanya mikutano 84. Huku akiweka wazi kwamba idadi hiyo ya watu wanaotarajiwa kufikishiwa elimu na mikutano hiyo ni tangu shirika hilo lianze kushirikiana na kuwa miongoni mwa vituo vilivyo chini ya shirika la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto wa Lindi(LIWOPAC), tangu mwezi Agosti,mwaka 2019.
Post a Comment