Bilioni 127 zatolewa kuchangia mfuko wa afya wa pamoja nchini
Wadau wa mfuko wa Afya wa pamoja (HBF) wanaofadhili upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya jamii wachangia Shilingi Bilioni 127 ili kuboresha huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipofany ziara na wadau wa maendeleo wanaochangia mfuko wa afya wa pamoja walipotembelea Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.
“Wenzetu hawa wanaochangia mfuko wa afya wa pamoja ambao ni wadau nane mwaka huu wa 2019/20 wametuopatia Bilioni 127 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 104 zitapelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya na Sekretarieti za Mikoa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ngazi ya Jamii huku kiasi cha Shilingi Bilioni 23 kikitarajiwa kutumika kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wa mfuko wa afya ngazi ya juu.
“Kwa hiyo tunaona hapa fedha nyingi zitakuja huku chini kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitli za Wilaya, nawashukuru sana wadau wetu wa maendeleo kwa kutupatia Bilioni 127 kwa ajili kuboresha huduma za Afya Tanzania” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi Mette Norgaard Dissing Spandet amesema kuwa mfuko huo umekuwa ukisaidia uboreshaji wa huduma za afya ngaza ya jamii kwa miaka 20 sasa na wanajivunia kuwa na uhusiano wa karibu na kusaidia katika upatikanaji wa bora huduma za afya nchini.
“Tunafuraha kufikia miaka 20 ya kusaidia katika kuboresha huduma za afya nchini Tanzania na tutaendelea kufanya hivyo zaidi kwa miaka mingi inayokuja” amesema Balozi Mette Spandet.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi ambaye Jiji lake ni mnufaika wa mfuko huo wa pamoja wa afya amesema kuwa walipokea fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 na walizitumia vizuri kwa kuboresha na kujenga miundombinu katika Kituo cha Afya hapa Hombolo.
“Kwa shilingi Milioni 500 tumeweza kujenga nyumba ya mganga, jengo la kuhifadhi maiti, jengo la upasuaji pamoja na jengo la wodi ya kina mama” anasema Mkurugenzi Kunambi.
Post a Comment