Maamuzi yatakayokusadia kubadili maisha

Ni maamuzi gani makuu matatu, ambayo ni muhimu kwa ubora wa maisha yako? 
Maamuzi ambayo yanasababisha wewe  kuandaa mazingira ya utajiri au umaskini katika muda wowote ule maishani mwako? Majibu ya maswali haya sio siri na pengine sio mageni masikioni mwetu, ila yanahitaji usikivu, ufuatiliaji, na umakini katika ufaniukishaji wake. Hivyo basi, zingatia maamuzi haya makuu matatu yafuatayo, ili uweze kubadili muelekeo wa maisha yako sasa hivi: 

Kuwa na Malengo Yanayoeleweka 
Kuna ule usemi usemao “Mgaa gaa na upya hali wali mkavu!” Ndugu zangu huu ni msemo mzuri kutoka kwa wahenga, lakini kama utakuwa unaamka asubuhi kila siku na kuingia mtaani kwa mtindo wa “kugaa gaa”, basi jua kwamba ni ngumu kufanikiwa, kwasababu hauna lengo linaloeleweka, yaani kwa ufupi unabahatisha, na katika ubahatishaji kuna kupata na kukosa na kama sio “mtu wa bahati” ndio hivyo tena Kwa mfano kama unataka kufanya biashara, basi panga sasa hivi ni biashara gani unataka kufanya, na fanya uchunguzi wa mambo yote yanayohitajika ili kuanza biashara hiyo. 

Tafadhali tuwe wakweli katika hili, kwani tusije tukajidanganya kwamba linalohitajika ni kufikiria tu biashara ya kuanzisha, la hasha! Anzisha biashara, ambayo ipo ndani ya uwezo wako kwasasa na hakikisha unaipenda hiyo biashara na isimamie kwa nguvu zote mpaka mwisho. Kama mtaji wako ni laki 2 (zaidi au chini ya hapo), na hauna namna nyingine yeyote ya kukuza mtaji huo, basi sio mwisho wa dunia, wewe anzia hapo hapo ulipo kwa kufikiria nini kinaweza kikafanyika kwa mtaji huo ulio nao. Mtaji mkubwa hauji kwa ndoto, anza kupanga mambo na kufanya sasa, kwani wahenga walisema pia hata “Mbuyu ulianza kama mchicha.” 

Kama wewe ni muajiriwa, basi fanya kazi kwa bidii sana, kiasi kwamba huyo muajiri wako inafika mahala anaona biashara yake haiwezi kwenda tena bila wewe kuwepo. Muda si mrefu utapandishwa cheo chenye malipo zaidi au amini usiamini waajiri wengine wataona uchapaji kazi wako, na watakuhitaji katika biashara zao kwa donge nono zaidi. Hivyo basi, mwisho wa siku, uchapaji kazi unalipa iwe hapo ulipo sasa au sehemu nyingine yeyote. Usiwe mtu wa kwenda kazini kwa lengo la kwenda tu, ili mshahara wako uingie mwisho wa mwezi, unatakiwa uende kazini na kuichukulia kazi yako kama mali yako binafsi na hapo ndio mafanikio huanzia. 

Chukulia Changamoto za kimaisha Katika Mtazamo Chanya 
Pindi unapopoteza kazi au biashara, pindi unapopata ajali, pindi unapofiwa na mtu muhimu maishani mwako, au pindi unapopatwa na janga lolote lile maishani, ni nini haswa unachofikiria? Je unafikiria huo ndio mwisho wa maisha yako au mwanzo? Jinsi tunavyochukulia vitu (kwa lugha sahihi) vinavyoitwa “changamoto” (sio “matatizo”) ni muhimu sana kwani tofauti ya mitazamo ina athari kubwa sana katika mustakabali mzima wa maisha yetu. Chukulia vitu hivyo vilivyotangulia kutajwa hapo juu kama changamoto, ambazo zinakukomaza wewe kimaisha, hii ni pamoja na kukosolewa na wengine. 

Kama mtu anakukosoa katika kile ufanyacho, basi usione hatari, kwani kukosolewa ni sehemu ya maisha na usione kila anayekukosoa ni adui yako. Kuna mambo mengi sana ya kujifunza kutoka kwa wale tunaowaita “maadui” zetu. Jifunze kufaidika na kunufaika kutoka kwa “maadui” zako, kwani kwa kiasi kikubwa ndio watu pekee (marafiki na wapambe walio wengi hupenda kutafuna maneno kwa kuhofia kukukera) ambao wapo tayari kutumia mapungufu yako ya kibinaadam kukushambulia, na unaweza ukatumia fursa hiyo kuimprove kwa faida yako. 

Jizuie Kufanya Maamuzi Yeyote ya Msingi Wakati Una Hasira 
Wahenga pia walisema “hasira hasara!” Hivi umeshawahi kuzingatia usemi huu kwa makini? Watu wengi hujikuta wakifanya maamuzi mazito maishani mwao kipindi ambacho wana hasira kutokana na kwamba kama binaadam hili ni rahisi sana kutokea. Lakini, sio lazima litokee kwako pia kama utaanza kujizowesha sasa kuzuia kufanya maamuzi yeyote ya msingi kipindi ambacho una hasira. Mke, mume, mteja, rafiki, na kadhalika…wanaweza wakakupandisha hasira na utakuwa na kila haki na sababu ya kukasirika, lakini hakikisha maamuzi yeyote unayotaka kuchukua dhidi yao, yawe ni maamuzi ambayo umeyafanya kipindi ambacho hasira zimetulia kama maji ya mtungi na mara nyingi huo ndio uwamuzi sahihi

No comments

Powered by Blogger.