Jinsi kauli yako inavyoweza kugharimu penzi lako

Kukosea katika uhusiano ni kawaida kabisa, naweza kusema ni sehemu ya maisha, lakini pia ni vizuri kuhakikisha kuwa unakuwa makini ili usikosee kila wakati. 

Hata hivyo, inawezekana kuwa makini na kujitahidi kutomuudhi mpenzi wako. Hilo linawezekana ikiwa utakuwa makini na kutambua mpenzi wako anapenda vitu gani na anachukia vitu gani. 

Baada ya kufahamu kuwa jambo fulani halipendi, ni vizuri ukaacha kabisa kutumia kauli hizo mbaya ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kukusababisha kukosana na mpenzi wako, hivyo kusababisha doa katika penzi lenu. 

Kuna baadhi ya watu wakiwakosea wapenzi wao, si  wepesi kukubali makosa na kuomba radhi, badala yake huendelea kuwa wakatili wasiotaka ushauri wa aina yoyote. Hayo ni makosa. 

MAKOSA YAMEHALALISHWA? 
Hapana! Hayajahalalishwa ila ijulikane wazi kuwa makosa katika maisha ni hali ya kawaida kabisa, usishangae kuwa na makosa katika uhusiano ni hali ya kawaida ambayo huweza kutokea si tu katika uhusiano bali hata maisha ya kila siku. 

NINI CHA KUFANYA? 
Hapa naweza kusema kuwa ndiyo penye mhimili wa mada yetu ya leo, kwakuwa kukosana ni jambo la kawaida katika uhusiano, basi lazima ifahamike jambo mbadala la kufanya baada ya kutokea mtafaruku katika uhusiano. 

Ikitokea umemkosea mpenzi wako na ukajua wazi kuwa ni kweli umemkoesea, ni wajibu wako kumuomba msamaha. Hata kama wewe ni mwanamume, kwa sababu wanaume hujiona wao kuwa ni vidume kwa hiyo hawaoni sababu ya kuomba msamaha pindi wanapowakosea wapenzi wao. 

Naweza kusema huo ni ulimbukeni usio na maana, kwani kusema samahani utapungua wapi ndugu zangu? Sema nisamehe mpenzi wangu ni hali ya kawaida, nilipitiwa kidogo! 

Bila shaka mpenzi wako atakuelewa na kukusamehe na maisha yataendelea kama kawaida. Usijijengee ujeuri katika mapenzi, huna jeuri yoyote katika mapenzi, kwani ukifanya jeuri itasaidia nini katika maisha yako? 

Hata kama wewe ni mzuri sana, lakini unatakiwa kutambua nafasi yako kwa mpenzi na nafasi ya mpenzi wako kwako. 

Tumia kauli nzuri na umfanye atambue kuwa hukufanya makusudi bali ulimkosea kwa bahati mbaya. Onesha jinsi unavyojuta kutokana na wewe kumkosea, bila shaka baada ya kugundua kuwa ulimkosea kwa bahati mbaya  lazima atakusamehe. 

KAULI CHAFU AU NJEMA? 
Hapa kuna jambo jipya kidogo, inawezekana kwa kuwa wewe ndiye uliyekosewa na mpenzi au wewe ndio mkosaji, ukatatizika na aina ya kauli inayokupasa kuitumia kwa ajili ya mpenzi wako na mkafikia mwafaka mzuri wa kupendeza. 

Hata kama wewe ndiye umekosewa huruhusiwi kabisa kutumia kauli chafu/kali kumweleza mpenzi wako jinsi ulivyochukia, badala yake unatakiwa kuwa mtulivu na kauli nzuri mbele ya mpenzi wako. 

Mweleweshe kwa upole, tena ukitumia kauli ya upole inakuwa rahisi kukuelewa na kuomba radhi, hali itakayorudisha maelewano baina yenu. 

Pamoja na hayo yote unyenyekevu wakati wa kuombana msamaha unahitajika sana, ni vizuri kuwa na unyenyekevu na utulivu wa hali ya juu wakati unapomwomba msamaha mpenzi wako ili mambo yaweze kwenda sawa. 

Ni vizuri wapenzi kuwa na kauli nzuri inapotokea kuhitilafiana, mkumbuke kuwa kukosana ni kama sehemu ya mapenzi. 

Epuka kuwa na hasira sana wakati wa kuzungumza juu ya tofauti zenu. Maneno makali ya kuropokeana si mazuri kabisa wakati mnawekana sawa, kauli njema zitumike ili mambo yaweze kuisha bila kusababisha matatizo mengine mapya. 

Suala la kukoseana katika maisha ni jambo la kawaida, si hivyo tu bali hata katika uhusiano. Lazima tukubali kuwa makosa yapo, mpenzio anapokukosea isiwe jambo la kushangaza sana, tambua kuwa ni hali ya kawaida ambayo unatakiwa kuikubali kwa hali yoyote. 

Kuwa na moyo wa kusamehe pindi mpenzi wako anapokukosea na kukuomba msamaha. Tambua kuwa anakuomba msamaha kwakuwa anatambua kuwa alifanya makosa na hakufanya kwa makusudi. 

Kubwa zaidi ambalo linapaswa kuzingatiwa ni kwamba utakapomkosea mpenzio na kumuomba radhi, basi hakikisha kuwa hurudii makosa.

No comments

Powered by Blogger.