Ubunifu kwenye teknolojia ukiongezeka tatizo la ajira litapungua
Kujenga uchumi imara kwa zama za leo, Benki ya Dunia inashauri kuwekeza kwenye ubunifu wa kisayansi.
Kwenye ripoti ya mwaka ya tathmini ya ubunifu katika sayansi na teknolojia ijulikanayo kama ‘Dar es Salaam ecosystem tech startup 2017’ benki hiyo inasema kuna fursa kemkem za kukuza uchumi wa taifa na kuimarisha kipato cha wananchi kwa ujumla endapo kutakuwa na mazingira rafiki kuufanikisha.
Endapo changamoto zilizopo kwa sekta hiyo zitafanyiwa kazi; kilimo na nishati jadidifu vitakua kwa asilimia 27 kila moja, ajira zitaongezeka kwa asilimia 22 wakati kurejeleza (recycling) kukiongezeka kwa asilimia 15 na Tehama ikiimarika kwa asilimia tisa.
Ingawa kilimo kina ajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wote lakini ukuaji wake ni chini ya asilimia nne kwa mwaka wakati Pato la Taifa likifanya hivyo kwa wastani wa asilimia saba ndani ya miaka mitano mfululizo. Bado vijana hawajahamasika kujihusisha ncho kutokana na kuendele akutumika kwa jembe la mkono, miongoni mwa sababu zilizopo.
Ripoti ya mwezi huu ya benki hiyo hiyo kuhusu uzalishaji na matumizi ya nishati jadidifu, iliiweka Tanzania juu kwa Afrika nzima kutoka na wingi wa miradi binafsi ya uzalishaji wa umeme huo hasa kutokana na nguvu za jua. Tanzania inayo miradi 109 ya nishati jadidifu inayohudumia zaidi ya wananchi 184,000. Sekta hiyo na fursa ya kukua kwa kasi hiyo endapo ubunifu utatumika.
Serikali inahangtaika kuhakikisha zaidi ya wahitimu 700,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka wanapata kazi. Idadi hiyo ni kubwa kuliko uwezo wa soko kuajiri lakini ripoti hii inaonyesha matumaini ya kupunguza uhaba uliopo.
Utafiti huo uliowashirikisha wajasiriamali 221 wa jijini Dar es Salaam kati ya Julai na Septemba mwaka jana unaonyesha kampuni 12 za wabunifu huanzishwa kila tangu mwaka 2009. Nyingi ni ndogo zinazoajiri wastani wa wafanyakazi wanne kila moja.
Urejelezaji wa vitu mbalimbali ni suala linalotiliwa mkazo kuanzia kwenye taka ngumu, mifuko ya plastiki, mabaki ya mazao hata uchafu wa bidhaa za kielktroniki. Hatua kadhaa zisizohusisha ubunifu zimekuwa zikitumika kufanikisha udhibiti wa bidhaa hizo kama ilivyokuwa vita dhidi ya pombe za viroba iliyolenga kukabili vifungashio vyake miongoni mwa sababu nyingi. Licha ya kukua kwa kasi kwa sekta ya Tehama nchini kunakochagizwa na ongezeko la televisheni za mtandaoni, tovuti binafsi, umma na kampuni, blogu na mitandao ya kijamii, bado kuna fursa nyingi, ripoti hii inasema.
Uwekezaji unahitajika ukifanyika na urasimu uliopo ukiondolewa, kwenye kila watu 100; 27 watapata fursa kwenye kilimo na wengine kama hao kwenye nishati wakati 22 wakiajiriwa kila mwaka. Urejelezaji utatoa nafasi kwa watu 15 na Tehama watu tisa. Tanzania itakuwa imefanikiwa kuajiri wananchi wake wote ikifanya hivyo.
Elimu na mafunzo
Tofauti ya maendeleo kati ya nchi zinazoendelea dhidi ya mataifa makubwa kiuchumi unatokana na matumizi ya teknolojia mpya inayoongeza tija katika uzalishaji. Eneo hili pekee linachangia tofauti hiyo kwa kati ya asilimia 70 mpaka 80.
Wabunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wanaelezwa kuwa muhimu kubuni teknolojia itakayoendana na mazingira pamoja na ufahamu wa watumiaji na kuziba ombwe lililopo katika maendeleo. Kuyapata maendeleo yanayohitajika, ubunifu wa ndani unahitajika badala ya kutegemea kununua teknolojia kutoka nje hasa mataifa ya magharibi. Kufanikisha hilo, wabunigu wanasema wanahitaji kuwezeshwa mtaji, utafutaji wa masoko, mafunzo na elimu.
Asilimia 42 ya waliosailiwa walisema wanakabiliwa na changamoto ya mtaji. Inaelezwa, taasisi za fedha nchini hazitoi kipaumbele kwa kundi hili hivyo kulinyima fursa ya kuongeza mchango wake kwenye vita dhidi ya umaskini wa kipato.
Mmoja katika kila wabunifu wanne nchini anapendekeza kuongezwa kwa sehemu za kufanyia mazoezi kwa vitendo. Jiji zima, kuna vituo vitano vinavyobainishwa kutoa mafunzo kwa wabunifu hawa.
Vinatajwa kuwa ni Buni Hub na Dar Teknohama Business Incubator (DTBI) vilivyopo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (Sido). kituo kingine ni Kinu Innovation Hub pamoja na kinachoendeshwa na Benki ya NBC.
Fursa
Utafiti huo unaeleza wabunifu wengi ni wahitimu wa chuo kikuu wenye uwezo wa kutatua kero mbalimbali zilizopo kwenye jamii. Asilimia 80 wana shahada ya kwanza wengi kwenye uhandisi na teknolojia, asilimia 15 wana shahada za uzalimi na wanaobaki ni wabobezi wa maeneo tofauti.
“Wahitimu wengi wanakosa uzoefu wa biashara kusimamia miradi yao…endapo jamii, washauri au walezi wa kibiashara na mazoezi zaidi ya kujaribisha ubunifu wao watachangia zaidi maendeleo ya taifa kwa ujumla,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Kuongeza ushiriki wao, maeneo kadhaa yanahitajikufanyiwa kazi. Kwanza ni taasisi za fedha kuiona fursa iliyopo kwenye sekta hii inayokua kwa kasi na kuweka mazingira rafiki ya kuikopesha. Masharti yapunguzwe na vijana hawa waaminiwe.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) nao unashauriwa kuongeza ofisi zake mikoani. Inaelezwa kuwapo kwa changamoto kwa wabunifu kila wanapotaka kusajili kampuni zao hasa waliopo nje ya Dar es Salaam ambako ofisi za Brela zinapatikana.
Kutopatikana kwa ofisi za Brela mikoani, kunaelezwa kuchelewesha maendeleo ya kampuni za kibunifu. Inaelezwa huwa rahisi kwao kufungua akaunti ya benki kuliko kusajili kampuni.
Hili linaenda sambamba na kupata ofisi kwani wapangishaji wengi wanataka kodi ya zaidi ya miezi mitatu ilipwe kabisa ilhali kampuni haijaanza kuingiza mapato na haijaajiri hata mfanyakazi mmoja.
Ukiacha mikopo ya benki ambayo huchukua mmpaka miezi minne kupatikana kwa kampuni hizi, kodi ni eneo jingine linalohitaji kufanyiwa kazi ili kuharakisha mchango wa sekta hii.
“Kodi na, sera sheria zake si rafiki kwa kampuni zinazoanza. Kupata wataalam wa kuandaa makadirio ya kodi ni ghali. Kupata baadhi ya vibali ni mlolongo mrefu. Kuna kasi ndogo ya kukamilisha taratibu zilizopo wakati mwingine bila sababu za msingi,” inasema ripoti hiyo.
Benki hiyo inashauri jamii kuziona fursa na kuwaunga mkono wabunifu hawa. Wajengewe uwezo kitaaluma kwa kupewa mafunzo sambamba na uzoefu wa biashara.
Kuongeza ufanisi hilo, benki inashauri wabunifu mmaarufu kimataifa waalikwe nchini na kukutanishwa na vijana wachanga ili kuchota uzoefu wao.
Kamisheni ya Tehama
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Teknolojia ya Mawasilino, Samson Mwela anaunga mkono matokeo ya utafiti huo na kueleza kwamba hatua zinachukuliwa kuhakikisha sekta hii inaongeza mchango wake kwenye uchumi wa taifa.
Anasema kuna mambo matatu ambayo kamisheni yake inayapa kipaumbele kufanikisha malengo hayo.
Kwanza, anasema ni kuwa na wataalamu wetu watakaotengeneza programi zitakazotatua kero zetu.
“Huwezi kutumia programu iliyotengenezwa India kwa mfano kutatua changamoto za Tanzania kwa sababu tunatofautiana,” anasema Mwela.
Jambo jingine ni kuimarisha soko la bidhaa za Tehama; programu na zana na vifaa vya kompyuta ili kukuza kipato cha wabunifu. Kufanikisha hilo, anasema watalaamu waliopo wanapaswa kuzalisha bidhaa za kutosha mahitaji ya ndani kabla ya kuanza kuuza nje ya mipaka.
Kupata wataalamu wa kutosha, anasema upo mpango wa kujenga vituo vya mafunzo kwa wabunifu hawa maeneo tofauti nchini.
“Huko ndiko watakaokutana na wawekezaji wa ndani na nje. Kutengeneza software unahitaji kufanya uwekezaji wa kutosha,” anasema Mwela.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Hassan Mshinda anasema taasisi na kampuni nchini zinapaswa kuziamini na kuzitumia bidhaa za wabunifu hawa.
Post a Comment