Baadhi ya mitindo ya nywele kwa kina dada

Mwanamke ni kiumbe ambaye anapenda kupendeza daima. Hii ndio tofauti kubwa kati ya wao na wanaume. Hatumaanishi kuwa wanaume hawapenda kipendeza, la hasha, ila katika safu hii siku ya leo tutaangazia nywele za kike. 

Nywele ni kiungo wazi kwa mwanadamu, wakati wanaume hupenda kuzikata wanawake hupenda kuzifuga kwa kuzisuka mitindo aina kwa aina. Kusuka nywele ni jambo la kawaida sana kwa wanawake wa Afrika. Lakini siku hizi hata Wazungu wengi hupenda kusuka nywele zao, na hii imeonesha kwamba wamehusudu aina hii ya urembo. 

Tangu enzi za mabibi zetu, wakati huo wakiwa wasichana vigoli walipenda kusuka ili kupendeza mbele za macho ya watu. Tofauti na sasa wao hawakuwa na mitindo mingi, ila kwa sasa tunashuhudia mitindo anuai vichwani mwa dada zetu. Na mitindo yote hii ina majina yake. 

Tukiachana na kusuka, pia kuna kuweka dawa za aina mbalimbali na kuzifanya nywele ziweze kufuata jinsi mwenye nazo atakavyo. Licha ya kuwa ni urembo lakini swala hili limetoa ajira nyingi kwa akina dada. 

Hebu basi tuone picha mbalimbali za misuko na mitindo ya nywele, na ukipenda usisite kujongea saluni yoyote ya karibu ili urembwe urembeke. 

Kwa kweli si kila kichwa kinafaa kusuka, lakini kama wewe unajua kuwa ukisuka unakuwa mwaaa, basi fanya hivyo. Tafuta fundi mzuri anayeweza kukushauri mtindo bomba wa kusuka kadiri ya kichwa chako kilivyo. 

Hii ni mitindo michache sana ya kusuka nywele, lakini ipo mingi mingi mingi ajabu, nawaahidi siku moja kuwalete fundi wa nywele kupitia JAMVI MEDIA ili mumsikie kwa masikio yenu akieleza juu ya urembo huu wa kiafrika. 

Nywele zina umuhimu sana kichwani na kila mtu anajua hilo, hivyo hazina budi kutunzwa kwa uangalifu. 

KUTIA DAWA NYWELE 

Ukiachana na habari ya kusuka, pia akinadada wengi hupenda kutia dawa kwenye nywele ili kuzifanyia aina nyingine ya urembo kwa ‘setting’. 

Miaka ya themanini hivi nakumbuka wakati huo dawa za nywele hazikuwa nyingi sana, zaidi ya kusuka, ili kuonesha urembo akina dada walikuwa wakichoma nywele kwa kutumia chanuo la chuma. Chanuo hilo lilipashwa moto kisha kupitisha kwenye nywele na baada ya hapo mafuta yalihusika na kufanya kichwa king’ae kweli kweli. 

Miaka ilivyozidi kwenda kikaja kitu kinaitwa Zazuu. Hii ilikuwa ni moja ya dawa za mwanzo sana iliyopakwa kichwani na kupendezesha nywele kwa kuzipa mwonekano chanya. 

Dunia ilipzidi kusogea, kukaja mtindo wa ‘Curl’, hii ilizifanya nywele kujipinda na kujizungusha kichwani. Wakati huo ndipo tukaanza kuona matangazo kwenye vyombo vya usafiri kuwa ‘Usiegemee Kioo’. 

Lakini katika ulimwengu wa sasa, kuna madawa mengi ya nywele mabaya kwa mazuri ambayo hutumika kupendezesha dada zetu. 

Hakika kwati ya wanawake kumi basi ni saba watakuwa wameweka dawa katika nywele zao. Nywele zilizowekwa dawa hukubali kila mtindo kichwani. Hebu tazama picha hizi: 


Kuna aina nyingi sana za kubana na kuseti nywele zenye dawa. 

Jumamosi ijayo tutao jinsi gani ya kuweka dawa kwenye nywele na aina ya mafuta mazuri kutumia kwa nywele zako. Pia tutatazama utunzaji na uoshaji wa nywele hizo.

No comments

Powered by Blogger.