Rais Emmanuel Macron asema Ulaya inapaswa kujiimarisha na kuzuia machafuko duaniani

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwamba Ulaya inatakiwa kujiimarisha na kushikamana zaidi ili kufanikisha jukumu lake la kuzuia kile alichokiita “machafuko” katika masuala ya kimataifa. 

Macron ameyasema hayo alipokuwa akilihutubia bunge la Ujerumani na kuongeza kwamba Ulaya, na ndani yake Ufaransa na Ujerumani wana jukumu la kuiongoza dunia kutoingia kwenye machafuko na kuwapitisha kwenye njia iliyo sawa na kuongeza kuwa ndio maana Ulaya inapaswa kuwa imara zaidi. 

Badaye Macron alikutana na Kansela Angela Merkel katika mazungumzo yao ya pamoja kuonyesha umoja dhidi ya kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo hususani wakati huu wa utawala wa rais Donald Trump wa Marekani. 

Viongozi hao wanaokutana kwa mara ya pili katika kipindi cha wiki moja wanatarajiwa kwa mara nyingine kuliibua suala la kuanzishwa kwa jeshi la pamoja la Ulaya pendekezo lililomghadhabisha sana Rais Trump. 

Ziara hii ya Macron inakuja wiki moja baada ya viongozi wa dunia kukutana mjini Paris Ufaransa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kumalizika kwa vita vya kwanza vya dunia na hii leo ameshiriki siku ya maombolezo nchini Ujerumani maalumu kwa ajili ya wahanga wa vita hivyo.

No comments

Powered by Blogger.