Mkwabi aahidi usajili wa kimataifa Simba
Mgombea pekee wa nafasi ya urais wa Simba, Swedy Mkwabi amesema kama akifaniiwa kushinda nafasi hiyo ameahidi kusimamia usajili wa kisasa ili timu hiyo ifanye vema kwenye michuano ya kimataifa Afrika.
Simba inatarajiwa kufanya uchaguzi wake Jumapili hii kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Posta jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo, mwaka huu inatarajiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na tayari imeanza maandalizi ya michuano hiyo kwa kukiboresha kikosi hicho kwa kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa.
Mkwabi alisema timu hiyo imeshiriki michuano ya kimataifa mara kadhaa na kuishia katikati, lakini kama akiingia madarakani yeye, basi anataka kuona timu hiyo ikichukua ubingwa wa michuano hiyo mikubwa Afrika.
Mkwabi alisema, mara atakapoingia atakutana na Kocha Mkuu wa timu hiyo Mfaransa, Patrick Aussems kwa ajili ya kujadili ripoti yake ya usajili na baadaye kukutana na bodi ya timu.
“Mara nyingi tumekuwa tukishiriki michuano ya kimataifa Afrika bila ya mafanikio ya kuchukua ubingwa, lakini mwaka safari hii anataka kuona timu hiyo ikichukua ubingwa huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Hilo linawezekana kama maandalizi tukiyaanza mapema kwa kuwaachia benchi la ufundi lifanye kazi vizuri bila ya kuingiliwa na mtu yeyote.
“Katika kuhakikisha timu yetu inachukua ubuingwa huo, ni lazima tuwe na kikosi imara kitakacholeta ushindani mkubwa kutokana na ukubwa wa michuano hiyo,” alisema Mkwabi aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo.
Post a Comment