Madhara ya kujamiiana kinyume na maumbile


TANGU asili binadamu hujamiana kwa mwingiliano wa uume kupitia njia ya ukeni na si kinyume na maumbile. 

Tendo hili ni la kiasili kwa wanyama wote wenye miguu minne, akiwamo binadamu. Umewahi kuona wanyama wakifanya hivyo kinyume? Jibu ni hapana kwa sababu sio asili yao. Watu wanaofanya hivyo huainishwa kama wenye matatizo ya afya ya akili na kitabia na hushauriwa kufika katika huduma za afya kwa matibabu na ushauri. 

Sababu za kufanya hivyo ni kutokana na kuiga, unyanyasaji wa kijinsia, matatizo ya kiakili, utunzaji wa ubikira, kukosa uhusiano, kukinai au kukosa hamu ya njia ya kawaida, ushawishi wa makundi, imani na mila potofu. 

Kujamiana kwa mtindo huu ni njia hatarishi sana inayochangia kuenea kwa maambukizi kirahisi, ikiwamo virusi vya Ukimwi, homa ya ini, Papiloma, Herpes na magonjwa ya zinaa ikiwamo kaswende. 

Eneo la njia ya haja kubwa maumbile yake ni kwa ajili ya kuhifadhi na kukitoa kinyesi, huwa na misuli migumu iliyo kama duara inayojifungua na kubana baada ya kinyesi kutolewa. 

Kitendo cha kujamiana kwa njia hii yenye misuli hiyo, ina maana kuwa upitaji unakuwa ni mgumu, kulazimisha kupenya husababisha majeraha yanayoambatana na maumivu makali. Hapo baadaye kuingiliwa mara kwa mara husababisha misuli hiyo kuwa dhaifu na kushindwa kudhibiti kinyesi hivyo kuweza kutoka chenyewe. 

Njia ya haja kubwa ina maelfu ya neva za fahamu, ndiyo maana ikitokea vijeraha maumivu huwa ni makali sana. Vile vile zikisisimuliwa huleta hisia chanya lakini hazifikii zile za kujamiana kwa njia ya ukeni. 

Kawaida njia hiyo haina tezi zinazozalisha vilainishi kama ilivyo kwa uke hivyo kulifanya tendo hilo kutokuwa salama kutokana na kupata michubuko kirahisi. 

Mpitisho wowote kutoka nje ya mwili katika njia hii huweza kusababisha michubuko kwa ndani hivyo kusababisha bakteria na virusi kuingia kirahisi katika mzunguko wa damu. 

Tafiti zinaonyesha kuwa kujamiana kwa njia hii kunahatarisha mara 30 zaidi kupata VVU ukilinganisha na anayejamiana kwa njia ya ukeni. 

Maambukizi mengine ni kama vile Virusi vya Papilloma (HPV) vinavyosababisha sunzua au vichuguu juu ya ngozi (warts) na saratani ya njia ya haja kubwa. Ni kweli wapo wanaodhani kuwa kutumia vilainishi vya viwandani kama mafuta mazito ni salama, lakini bado havizuii michubuko kutokea katika njia hiyo. 

Ieleweke kuwa ndani ya njia ya haja kubwa hakuna ulinzi kama ule wa nje ya njia hiyo ambapo huwa na tando za seli zilizokufa ambazo huwa ni kizingiti kinachotoa ulinzi dhidi ya vimelea vya maradhi. 

Kutokuwa na ulinzi wa aina hii ndani ya njia ya haja kubwa husababisha hatari ya kupata michubuko kuwa juu hivyo kuenea kwa maambukizi kirahisi. 

Njia ya haja kubwa ndani yake kuna mamilioni ya bakteria ambao ni rafiki tu katika eneo hilo ila ni adui wanapohamishwa eneo hilo. 

Kujamiana kwa njia hiyo kunaweza kuwahamisha bakteria hao na kusababisha uambukizi katika uke na njia ya mkojo. 

Kuingiliwa kinyume na maumbile kwa mtu anayeugua Bawasiri, kunaweza kusababisha akavuja damu nyingi na kupata maumivu makali. 

Vilevile kuingiliwa njia hii kunaweza kusababisha kutoboka au kuchanika kwa utumbo mpana, jambo linalohitaji huduma za dharura kwani mtu anaweza kupoteza damu nyingi na kufa.

No comments

Powered by Blogger.