Waziri Mkuu aitaka SIDO kwenda na falsafa ya Hapa Kazi Tu
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lijielekeze katika kubuni teknolojia na mitambo rafiki inayolenga kutatua changamoto za wajasiriamali kulingana na mazingira yao.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za SIDO lakini bado kuna changamoto za wajasiriamali wadogo ambazo lazima zishughulikiwe kwa kasi kubwa ili kufungamanisha shughuli za SIDO na uchumi wa Viwanda
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Oktoba 23, 2018) wakati akifungua Maonesho ya SIDO kitaifa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nyakabindi ulioko wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na wajasiriamali 500.
Amesema ili kufikia uchumi wa kati inabidi kila Mtanzania mahali alipo afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu. “Tusipoteze wakati kwa kufanya mambo yasiyo na tija. Tuzingatie falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu.
“Mfano kwa hapa Bariadi, tunatarajia SIDO watuletee teknolojia na mitambo inayoweza kurahisisha ukamuaji wa mafuta yanayotokana na mbegu za alizeti na pamba, kwa Dodoma taknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata zabibu.”
“Kigoma pelekeni teknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata mbegu za michikichi na kwenye maeneo yanayolimwa korosho teknolojia na mitambo ya kubangua korosho na maeneo kama Ilula ambayo yanazalisha nyanya kwa wingi wapate teknolojia na mitambo ya kusindika na kuhifadhi nyanya na mbogamboga.”
Post a Comment