Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amezindua ujenzi wa Ofisi moja Kati ya ofisi mbili za kisasa alizoahidiwa na Kampuni ya Ujenzi ya CRJE iliyoguswa na Kampeni ya Makonda ya Ujenzi wa Ofisi 402 za Walimu Dar es salaam. 

Makonda amesema moja kati ya vitu vinavyomnyima usingizi ni pale anapoona walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu ikiwemo kufanya kazi chini ya miti na kwenye korido ndio maana ameamua kuanzisha Kampeni ya ujenzi wa ofisi nzuri na zakisasa kwaajili ya walimu ilikuhakikisha heshima ya walimu inarejea. 

Akizungumza katika uzinduzi uliofanyika shule ya Msingi Vijibweni Wilayani Kigamboni Makonda amesema uwepo wa mazingira bora ya kufanyia kazi kwa walimu Ndio chachu ya kuongezeka kwa ufaulu ambapo amewapongeza walimu na watendaji wa elimu kwa kuifanya Dar es salaam kuongoza kitaifa katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba. 

Makonda amesema ofisi hizo zitakuwa na mahitaji yote muhimu ikiwemo ofisi ya mwalimu mkuu, mwalimu mkuu msaidizi, ukumbi wa mikutano, ofisi ya walimu wote, chumba cha mitihani, chumba cha mhasibu,mapokezi, stoo, Vyoo na Bafu. 

Kwa upande wao walimu wa shule ya msingi Vijibweni wamemueleza Makonda kuwa shule hiyo haina ofisi yoyote ya walimu hivyo wamekuwa wakifanyia kazi chini ya miti na kwenye korido ambapo wamemshukuru kwa kuwaletea mfadhili wa kuwajengea ofisi ya kisasa.

No comments

Powered by Blogger.