MAMBO NILIYOYAONA SIMBA Vs YANGA LEO

1.Jonas Mkude. Yeye mwenyewe hujiita Master Plan. Hakika Jonas Mkude ni bwana mipango. Mipango yote ya Simba ilianzia kwake. Alikua kila kitu kwenye eneo la Kiungo. Alikaba na kuchezesha timu kwa umahiri mkubwa huku akiiunganisha safu ya ulinzi na ile ya ushambualiaji. Kuna wakati huwa najiuliza hivi ni nini kinachomkamisha kucheza soka la nje. Mkude ana uwezo mkubwa sana. Anajua nini anachokifanya uwanjani. 

2. Beno Kakolanya. Zile gloves alizozitumia leo haitaji kuzitumia tena. Nitamshauri hivyo kama nikiapata nafasi ya kuzungumza naye. Anatakiwa azitunze kama kumbukumbu. Yanga walifaidika sana kuwa nae pale golini. Kama isingekua yeye basi yale yaliyotokea mwaka 2012 yangeweza kujirudia tena. Wazungu husema neno moja fupi kwa kile alichokifanya "what a performance".Man of the match? Hakika ni Beno Kakolanya. Hakuna mjadala hapa. 

3. Ulimuelewa vizuri Mwinyi Zahera? Ulielewa alichokifanya?. Ngoja nikwambie Zahera alijua anakwenda kushindana na Simba iliyobora sana. Alichokifanya ni kuingia uwanjani na mbinu ya kujilinda zaidi. Alianza na mabeki wanne, akampanga Abdallah Shaibu kama kiungo wa ulinzi aliyekua na kazi ya kuvuruga zaidi, kisha akawaweka Feisal Salum, Papy Tshishimbi na Ibrahim Ajibu kama viungo akimuacha Heriether Makambo peke yake akisaidiwa na Deus Kaseke kule mbele. Wakati Yanga wanashambuliwa, alitengeneza msitari wa watu watano. Hapo ndipo ugumu ulipoanzia. 

4. Patrick Aussem. Anajaribu kuleta kitu kipya. Amekuja na mfumo wa 4-2-2-2. Hatujauzoea sana mfumo huu hasa kwenye soka letu la Kitanzania. Anachokifanya ni kuanza na mabeki wanne, viungo wawili wakabaji, viungo wawili wa ushambuliaji na washambuliaji wawili pia. Inahitaji muda kidogo kuweza kumuelewa. Anaifanya Simba kuwa timu imara sana. Imara kwenye kuzuia na imara kwenye kutengeneza mashambulizi. Bahati mbaya mambo bado sio mazuri kwenye idara ya ushambuliaji. Kuna wakati natamani sana kumuona Asante Kwasi kwenye mfumo huu. Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wanazihitaji sana krosi zake. 

5. Simba wana mtu anayeitwa James Kotei. Hana bahati ya kusemwa na kukubalika sana, lakini ngoja nikwambie kitu, Simba hawana kiungo mwingine anayejua kukaba kama James Kotei. Yeye ndiye aliyeirahisisha sana kazi ya Jonas Mkude na Cleutus Chama. Kotei anatambua yeye sio mzuri kwenye kuchezesha timu, anachokifanya ni kupokonya mipira na kumpatia Jonas Mkude, bwana mipango. 

6. Kwenye mziki wa bongofleva kuna Young Killer "Msodoki". Yanga wana Young Killer wao. Ni Feisal Salum "Fei toto". Akimuangalia Feisal anaonekana ni mwenye sura ya kitoto sana lakini hufanya kazi chafu sana pale katikati. Feisal amebarikiwa vyote, ni kiungo fundi anayejua kukaba. Angalau alikua akileta uhai kwenye eneo la kiungo la Yanga, bahati mbaya alikua akikutana na kina Mkude pale kati. Anazimwa. 

7. Ulimuona Cleutus Chama?. Yule ni kiungo fundi hasa. Anajua kutoa burudani. Bado nafikiria kama kuna umuhimu wa Haruna Niyonzima tena. Chama anafanya mengi ambayo Niyonzima alikua akiyafanya. Ilikua ni burudani sana kumuangalia akicheza, hasa kile kipindi cha kwanza. Ni kiungo mchezesha timu halisi. Alijua wapi anatakiwa kuupeleka mpira, alijua wapi anakiwa kutoa burudani tu ya soka. Msitari wa watu watano uliotengenezwa na Yanga chini ya Kamanda Kelvin Yondani uliharibu mipango mingi sana ya Chama. Kipindi cha pili akamua kutulia tu. Hakua na cha ziada cha kutuonesha. 

8. Abdul Shaibu. Haihitaji kufikiri mara mbili kutambua kwanini alipewa jina la Ninja. Yule ni Nina haswa. Mkatili ambaye hana muda wa kutabasamu anapokua uwanjani. Alicheza nyuma zaidi akiwalinda Kelvin Yondani na Vincent Andrew. Kazi kubwa aliyokua anaifanya ni kuharibu mipango yote aliyokua inatengezwa na Simba. Kwa muda mrefu sikuwahi kumuona mchezaji wa Kitanzania anajua kucheza tackling nyingi za kufanikiwa, bila kucheza faulo. Shaibu alilifanya hilo kwa ubora sana. Sikumbuki kama alipewa kadi. Ngoja nikaangalie takwimu. 

9. Ulimuona Herieter Makambo? Hakuwa na madhara sana kwenye eneo la ulinzi la Simba. Inahitaji darubini kuangalia kama alipiga angalau shuti moja kwa Aishi Manula. Unajua kwanini? Kwa sababu Ibrahim Ajibu alifichwa huku Gadiel Michael alikua bize sana kuwadhibiti kina Kichuya na Shomari Kapombe. Makambo ni mzuri sana kwenye mipira ya juu. Unapodhibiti mipira ya juu kumfikia unamfanya anakua mzururaji tu uwanjani. Deus Kaseke alijaribu kumtengeneza nafasi lakini alidhibitiwa vizuri na Kina Pascal Wawa. 

10. Uliona alichokifanya Ibrahim Ajibu mara baada ya filimbi ya kuanza mchezo ilipopulizwa?. Huku kwetu uswahilini kile alichokifanya tunakiita "Kufuata mashariti". Ukienda hospitali daktari husisitiza kufuata mashariti jinsi unavyotakiwa kunywa dawa. Ndicho alichokifanya Ajibu. Kule ilikua ni kutimiza mashariti kama nilivyozema. Asingefanya vile basi mambo yangekua tofauti sana.

No comments

Powered by Blogger.