Mwakyembe: Tutabaki wasindikizaji tu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ameutaka uongozi wa Baraza la Michezo nchini (BMT) kufuata yale yote yanayotakiwa katika utendaji kazi wao ikiwemo kutekeleza kazi za nyongeza alizowapa ili kuhakikisha michezo inakuwa nchini.
Waziri Mwakyembe amesema hayo hii leo Mei 08, 2018 wakati wa kuzindua Baraza la 14 la michezo ambapo amelitaka Baraza hilo kuhakikisha wanakuwa na mda wa kukutana na wadau wa michezo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wilaya na mikoa ili kuhakikisha vyama pia vinakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu michezo.
"Kutokana na hali halisi ya michezo hapa nchini kwetu, nimeamua kutoa kazi za nyongeza kwa Baraza ambapo kazi hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza na kuendeleza michezo hapa nchini, kubwa zaidi ya yote ni kulitaka Baraza kuhakikisha vyama vinaheshimu katika zao kwa kufanya uchaguzi ndani ya mda waliopanga ili kuweza kutoa nafasi kwa wanachama wao kuweza kusapoti mchezo huo na kuuendeleza", amesema Mwakyembe.
Pamoja na hayo, Waziri Mwakyembe ameendelea kwa kusema "hatuna budi kuwekeza kwa watoto ambao ndio watakaoweza kuinua michezo hapa nchini na bila hivyo daima tutabaki wasindikizaji kwa kila mchezo na tutakuwa tukilalamika tu bila kujua tunatakiwa kurekebisha wapi".
Kwa upande mwingine, Waziri Mwakyembe amesema ipo haja ya kuwekeza kwenye miundombinu ya kimichezo hapa nchini ili kuhakikisha watoto pindi wawapo katika viwanja vya michezo wanakuwa katika mazingira yaliyokuwa bora ya kimichezo.
Post a Comment