Umuhimu wa lishe bora kwa muathiika wa virusi vya UKIMWI
Lishe bora ni muhimu zaidi kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, kwani mahitaji ya miili yao kilishe yameongezeka kwa sababu ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Vilevile magonjwa mengi yanayoambatana na virusi vya UKIMWI huathiri ulaji, uyeyushwaji, usharabu ( ufyozwaji) na utumikaji wa virutubishi mbalimbali mwilini na hivyo kumuweka mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI katika hatari ya kupata matatizo yanayoambatana na lishe duni.
Ulaji bora wa vyakula mbalimbali huweza kuboresha afya na lishe ya mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI na hivyo huweza kuongeza muda wa kuishi. Lishe bora pia ni muhimu katika kusaidia dawa zinazotumika kuweza kufanya kazi vizuri. Ni muhimu kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kula mlo ulio kamili. Mlo ulio kamili husaidia kuboresha lishe na afya, na pia huweza kuboresha kinga ya mwili.
Binadamu wote wanahitaji chakula chenye kukidhi mahitaji ya kilishe ya miili yao. Chakula huupatia mwili virutibishi mbalimbali kwa ajili ya afya bora, ambayo ni pamoja na:
- Kuboresha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali;
- Kutengeneza na kurudisha seli za mwili zilizokufa, zilizochakaa au kuharibika;
- Ukuaji wa kiakili na kimwili; na
- Kuupa mwili nguvu, joto na uwezo wa kufanya kazi.
Post a Comment