Uvumilivu unatakiwa

 


Ukiwa mtu wa kuangalia mambo kwa juu juu basi kila kitu kwako kitakuwa kigumu. Kusoma unaweza kuona ni kugumu, kufanya kazi kugumu, hata kusubiri mshahara unaweza kuona ni kugumu.

Urahisi kwako unaweza kuwa katika kutumia pesa, pengine  na kula tu. Ila watu waerevu na wenye uvumilivu kwako kila kitu kinaweza kuwa tofauti na wewe.

1. Unachoona kigumu kwao wanahisi si ugumu bali ni changamoto za kuzidisha jitihada na umakini tu. Kwenye mapenzi pia hali haiko tofauti sana. Wale wanao achana kila siku si kama ndiyo wanakosewa sana kuliko wale ambao hawaachani, hapana. Suala ni lile lile tu.

2. Wakati wengine wakiona tofauti zao ni kama changamoto za kusomana tabia na kuamua kuishi kutokana na kila mmoja kumjua mwenzake. Wenzao wanaona suluhisho la yote ni kila mmoja kuwa na maisha yake. Suala la uvumilivu kwao hamna.

3. Hakuna mapenzi duniani yanayoweza kushamiri bila suala hili. Usipokuwa na moyo wa uvumilivu katika mapenzi basi kila mtu utamuona hafai. Utamuona hafai na kila siku utakuwa mtu wa kuanzisha mahusiano mapya. Hayo si maisha sasa!

4. Mahusiano yaliyodumu si kwa kuwa wahusika hawakoseani au makosa wanayokoseana ni madogo sana. Hapana. Kila binaadamu ana mapungufu yake. Wote huwa wanakoseana ila tofauti yake na wengine ni kwamba busara na uvumilivu huwa msingi wa mapenzi yao na ndiyo maana tunaona wanadumu mpaka leo.

5. Ni binaadamu gani unaweza kuishi naye na msikosane? Ni nani mwenye uwezo wa kukupa unachotaka kila siku? Hakuna binaadamu wa aina hiyo.

6. Hivyo unavyotaka kuachana na uliye naye suala la kujiuliza ni kuwa mara ngapi umemueleza kuhusiana na suala unalotaka kumuachia. Na hiyo isitoshte tu pia jiulize ni sababu gani inayomfanya kutenda suala hilo. Ukimaliza hapo rudi nyuma na jiulize tena huwa unatumia maneno ya aina gani katika kumkanya.

7. Maana wengine baada ya kukosewa wao huwa hawawakanyi vyema wenzao wao bali huripuka kwa maneno makali na dharau. Matokeo yake sasa wahusika badala ya kuwasikiliza na kufanyia kazi maneno wanayoambiwa kutokana na makosa yao. wao huwapuuzia na kwaona ni wasema hovyo.

8. Ndiyo, kukosewa kunaumiza sana ila jiulize ni kitu gani kimetokea bila sababu? Kwenye makosa ya mpenzi wako kuna sababu nyuma yake, hebu itafute badala ya kulalamika.

9. Mapenzi yasiyo kuwa na uvumilivu ndani yake hayana maisha marefu. Kwa sababu binaadamu ni kiumbe mwenye kukosea.

10 Badala ya kukimbilia kuachana ebu geuka kuwa mwalimu wa mpenzi wako angalau kwa mara chache.

11. Mpenzi wako ni furaha yako kwa maana ndiyo mtu uliyeridhia naye kuwa naye katika masuala nyeti yahusuyo maisha yako. Sasa kwanini uwe tayari kumpoteza kisa kachelewa kurudi.

12. Kuwa mvumilivu . Watu wenye hekima ni wavumilivu. Watu wenye kujielewa ni wavumilivu.

13. Ukiwa hauna uvumuilivu kila siku utatangaza ndoa. Leo utaachana na Mugambara kwa sababu anaongea sana na wasichana ila, jua huyo unaeenda kuwa naye anapenda sana kitu ambacho hukipendi. Anakunywa pombe je, utawezana naye? Jibu unalo.

14. Kwa kuwa huyo uliye naye unampenda kwa dhati basi amua kwenda naye taratibu ukijitahidi kumbadilisha tabia zake. Usiogope, inawezekana, suala ni uvumilivu na kujiamini tu. Kukubali kumpoteza unayempenda kwa kukosa uvumilivu ni kujitakia kuingia katika maisha ya kutanga tanga tu.

15. Kumbuka, siku zote wanaovumilia ndiyo huwa wanabaki na ushindi.Bila uvumilivu Mandela asingekuja kuwa raisi wa afrika kusini.Uvumilivu ni kila kitu katika maisha

No comments

Powered by Blogger.