Rais Mstaafu Kikwete ataka viongozi kuacha tabia ya kujikweza


Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete amewataka viongozi nchini kuachana na tabia ya kujikweza mbele za watu na badala yake kuishi kama binadamu wa kawaida kwani kwa kufanya hivyo hakuwapunguzii cheo walicho nacho.

Amesema watanzania hatutakiwi kubaguana kwa dini wala kabila na kwamba Mwalimu Julius Nyerere pamoja na ukubwa aliokuwa nao kama rahisi alikuwa mtu wa kawaida mbele ya watu wengine.

Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lililofanyika jijini Dar es Salaam.

“Ni jambo la muhimu viongozi kutambua kuwa kujishusha hakukufanyi usiwe kiongozi kwasababu una wakati wa kutimiza majukumu yako lakini unapokuwa na binadamu wenzako wako kama wewe,”.

“Orodha ni ndefu ya mambo ya mwalimu kwa sisi ambao tumebahatika kuwa karibu naye ametuachia urithi wa mambo mengi muhimu katika nyanja zote za maisha ya Watanzaniani sasa ni wajibu wetu kuutambua urithi huo na kuutunza, baadhi ya mambo hayo yameshakuwa tunu za taifa na ndizo zinazolea taifa hili,”.

 “Watanzania wenzangu, wanachama wenzangu wa CCM na vyama vingine vya siasa, wa rangi zote, makabila yote na madhehebu yote ya dini tushikamane katika kusimamia tunu hii, amani na umoja hauna kabila wala chama na mtu yeyote anayepuuza mambo haya haitakii mema nchi yetu wala yeye mwenyewe,” amesema Dk. Kikwete.

No comments

Powered by Blogger.