Mambo 12 yaliyotolewa na serikali kwa Wabunge leo


Jumatano hii, Februari 6, 2019, Katika kipindi cha maswali na majibu bungeni Jijini Dodoma,wabunge mbalimbali wameuliza maswali na kujibiwa na serikali. 

Tazama mambo muhimu kwa ufupi yaliyotolewa na serikali: 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira -Anthony Mavunde 

1. Serikali katika kutambua bodaboda kama moja ya usafiri wa kubeba abiria nchini Kisheri mwaka 2017 ilifanya marekebisho ya Kanuni za Usafirishaji za mwaka 2010 ambapo waendesha bodaboda walirasimishwa kwa kupatiwa leseni za Usafirishaji. 

Naibu Waziri  Ofisi ya Rais TAMISEMI - Mwita Waitara 

2.  Serikali imekuwa ikiongeza posho na maslahi ya Madiwani nchini kwa awamu kulingana na uwezo wa Halmashauri kukusanya mapato ya ndani. 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Sima 

3. Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 129(1) kinaeleza wajibu wa kila mamlaka ya serikali za mitaa kwenye eneo lake itajenga au kuandaa mifereji ya maji ya mvua. 

Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano-Elias Kwandikwa 

4. Kwa mujibu wa Sheria za Kimataifa za Usalama wa Anga, hairuhusiwi watu, wanyama, magari kukatiza kwenye viwanja vyovyote vya ndege. 

Naibu Waziri wa Kilimo-Innocent Bashungwa 

5. Serikali inatambua umuhimu wa mazao ya viungo kutokana na mchango wake katika kipato cha wakulima mmoja mmoja na pia katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni. 

6. Serikali imeandaa Mwongozo wa uzalishaji wa mazao ambao umebainisha maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya viungo. 

Naibu Waziri Kilimo Omary Mgumba 

7. Katika mwaka 2015/2016 Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania( TaCRI) imefanya utafiti wa gharama za uzalishaji wa kahawa katika Wilaya za Mbinga, Mbozi, Tarime, Rombo, Muleba, Karagwe na Buhigwe ambazo ni miongoni mwa Wilaya zinazozalisha zao la kahawa nchini. 

8. Katika kuboresha mazingira ya biashara ya zao ka kahawa, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuamua kuanzisha minada ya kahawa kwenye maeneo ya uzalishaji kuanzia msimu wa 2019/2020. 

9. Serikali imefuta tozo na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinatozwa kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo zilizokuwa zinatozwa katika biashara ya kahawa pamoja na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinakusanywa na Mkulima.

Naibu Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile 

10.Serikali inatambua Changamoto za uchangiaji wa huduma za afya na inaandaa utaratibu wa bima ya afya kwa watanzania wote ikiwa ni pamoja na kundi la walemavu. 

Naibu Waziri Madini Sospeter Nyongo 

11. Wizara ya Madini inaendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa leseni kuhusu uchimbaji bora wa madini ya jasi na kuwataka kuchangia miradi ya maendeleo katika jamii kwenye maeneo yanayozunguka migodi kwani ni takwa kisheria. 

12. Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kusafirisha umeme mkubwa  wa kilovoti 400 katika Mikoa ya Kusini Magharibi ikiwemo Mikoa ya Rukwa Katavi na Kigoma kwa lengo la kuwaunganisha wananchi wa wa maeneo hayo na gridi ya Taifa. 

No comments

Powered by Blogger.