Maradhi ya fizi na meno

Aina za maradhi ya fizi na dalili zake 

Kupiga mswaki na kutunza meno sio suala gumu na iwapo tutapiga mswaki ipaswavyo pamoja na kutumia nyuzi kusafisha katikati ya meno, tunaweza kuzua maradhi ya fizi na pia meno kuoza. Maradhi ya fizi husababishwa na utando kwenye meno unaotengenezwa na bakteria, ute na chembechembe nyinginezo zinazoganda kwenye meno. 

Kwa mujibu wa Taasisi ya Meno ya Marekani (ADA) iwapo utando katika meno hautaondolewa huwa mgumu na kuwa ugwagwa wa meno au tarter inayotumiwa na bakteria. Mchanganyiko wa utando na ugwagwa katika meno husababisha uvimbe kwenye fizi hali inayojulikana kitaalamu kama gingivitis. Ukoga wa meno au ugwagwa 

unaweza kundolewe na daktari wa meno au dentist.Maradhi ya fizi yana awamu tatu. Awamu ya kwanza kama tulivyosema ni gingivitis, ambapo fizi huwa nyukundu, huvimba na hutokwa na damu kwa urahisi. Iwapo hali hiyo itagundulika mapema inaweza kutatuliwa kwa kupiga mswaki vizuri na kutumia nyuzi kusafisha katikati ya meno.Awamu ya pili ya ugonjwa wa fizi ni hali ijulikanayo kama Periodontitis ambapo uvimbe hutokea kuzunguka 

jino. Awamu hii ni iliyoendelea zaidi ya ugonjwa wa fizi inayotokea wakati sumu ya bakteria katika utando inapoharibu fizi zilizoshikilia jino. Suala hilo husababisha fizi ziachane na jino na kutengeneza mada haribifu. Baadhi ya wakati mfupa ulioliwa kuzunguka jino unaweza kuonekana. Matibabu ya maradhi haya ya fizi ni muhimu sana ili kuzuia mmomonyoko wa mfupa na kung'oka meno.Awamu ya tatu ya maradhi ya fizi ni periodontitis iliyoendelea. Katika steji hii uharibifu wa fizi huwa mkubwa zaidi kuliko kabla na mfupa wa jino hulika. Pia meno huweza kung'oka na baadhi ya wakati huhitaji kung'olewa iwapo matibabu hayatosaidia. 

Dalili za maradhi ya fizi 

Hapa linajitokeza swali kwamba ni zipi dalili zinazojitokeza wakati mtu anapokuwa na ugonjwa wa fizi ulioendelea? Dalili za advanced periodontitis ni kuwa na harufu mbaya ya mdomo ambayo haiishi. Fizi kuvimba, kuwa nyekundu na laini. Dalili nyingine ni fizi kusogea mbali na meno, kuhisi maumivu wakati wa kutafuna na kupoteza hisia katika meno. 

Sababu za maradhi ya fizi 

Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kupatwa na magonjwa ya fizi. Miongoni mwa sababu hizo ni kuvuta sigara au kutafuna tumbaku. Mbali ya kuwa uvutaji sigara unaathiri mwili wa binadamu kwa njia tofauti, moja ya athari za ufutaji sigara hudhihirika katika kinywa cha mtu. Kwa kuwa moshi wa sigara 

hupita kwenye meno na fizi, kinywa cha mvuta sigara huwa kituo cha nicotine ambayo huharibu muonekano wa meno kwa kuyabadilisha rangi na kuacha harufu mbaya kinywani. Si hayo tu bali uvutaji sigara pia huathiri tishu za fizi na kupunguza mtiririko wa damu katika fizi, na kuleta uharibifu unaosababisha fizi zisogee mbali na 

meno.Wataalamu wanatuarifu kuwa, asilimia 75 ya watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa fizi ni watu wazima huku wale wanaovuta sigara wakiwa kwenye hatari ya kusumbuliwa na ugonjwa huo mara 7 zaidi ikilinganishwa na watu wasiovuta sigara.Sababu nyingine inayochangia katika kupata ugonjwa wa fizi ni mabadiliko ya homoni kwa wasichana na wanawake. Wanawake wako katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya kinywa na meno kuliko wanaume kutokana na mabadiliko ya homoni yanayosababishwa na maumbile yao. Sio tu mabadiliko ya homoni 

kwa wanawake na watoto huathiri mtiririko wa damu katika tishu za fizi, bali pia huchangia katika suala zima la kupatikana ugando kwenye meno au plague unaosababisha meno kuoza. Mabadiliko ya homoni huwafanya wanawake wawe kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa fizi wanapokuwa katika hali tofauti kwenye maisha yao ambazo ni wakati wa kubalehe, wakati wa hedhi, wanapotumia vidonge vya kuzuia mimba, wanapokuwa 

wajawazito na wakati wanapoacha kupata hedhi yaani menopause. Hayo yote husababishwa na mabadiliko yanayoshuhudiwa katika homoni za estrogen na progesterone kwenye vipindi hivyo. Kwa sababu hiyo tunaweza kusema kuwa, watoto wa kike, wasichana na wanawake kwa ujumla wanapaswa kuzingatia zaidi usafi na utunzaji 

wa fizi na meno ili kuepusha uharibifu wa meno unaowapata zaidi kutokana na jinsia yao kuliko wanaume.Sababu nyingine inayoweza kumfanya mtu apatwe na maradhi ya fizi ni ugonjwa wa kisukari. Madaktari wanatuambia kuwa, watu walio na ugonjwa wa kisukari ambao hawadhibiti vyema ugonjwa huo, wako katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya meno na maambukizi katika fizi. Hii ni kwa sababu ugonjwa wa kisukari hupunguza mtiririko wa 

damu kwenye fizi na pia kiwango cha juu cha sukari kwenye damu husababisha kinywa kiwe kikavu na kuzidisha ugonjwa wa fizi. Upungufu wa mate mdomoni huongeza bakteria wanaoharibu meno na kuleta utando. Iwapo mtu mwenye kisukari atadhibiti ipasavyo kiwango cha sukari kwenye damu, hatari ya kupata matatizo ya meno hupungua. 

Namna ya kuzuia maradhi ya fizi 

Suala muhimu zaidi linaloweza kuzuia mtu asipatwe na maradhi ya fizi na kuoza meno ni kupiga mswaki na kutumia nyuzi kuondosha uchafu katikati ya meno kwa uchache mara moja kila siku. Suala hilo linaweza kuzuia maradhi ya fizi, meno kutoboka na kung'oka. Licha ya kusafisha meno kila siku, jambo jingine muhimu ni kufanyiwa uchunguzi na daktari wa meno kwa uchache mara moja kwa mwaka. Hii ni kwa sababu hata kama tunajitahidi kwa kiasi gani kupiga mswaki, lakini mgando na ugwagwa hujitokeza na kusababisha matatizo katika fizi. 


Je, ni Namna gani tupige mswaki kwa njia iliyo sahihi? 
Kwanza kabisa tunashauriwa kupiga mswaki asubuhi na kabla ya kwenda kulala. Ikiwezekana piga mswaki baada ya kula chakula. Kama hauwezi, piga mswaki baada ya kula vyakula vya sukari. Tunapaswa kutumia mswaki laiini na wa wasitani, kwani mswaki mkubwa hautafika kwenye meno ya nyuma ilhali ule ulio mdogo utakufanya utumie 

wakati mwingi sana katika kusugua meno. Ikiwa unahitaji usaidizi katika kuchagua mswaki, pata ushauri kutoka kwa daktari wako wa meno. Tumia dawa ya meno iliyo na floraidi. Watoto wanapaswa kutumia kiasi kidogo cha dawa ya meno na watu wazima watie dawa ya meno kulingana na urefu wa nywele za mswaki.Wataalamu 

wanatushauri kubadilisha mswaki pindi ule tunaotumia unapochoka, kila baada ya miezi mitatu au minne. Pia tunashauri kuwa ni vizuri kubadilisha mswaki mpya kila baada ya kupata mafua, uvimbe katika koo na magonjwa mengineyo kama hayo. 

Kumbuka kusugua pande zote za meno kwa njia ifuatayo: 
Sugua meno yako polepole bila kutumia nguvu kutoka sehemu ya nyuma hadi mbele. Sugua karibu na ufizi kwa mwendo wa mviringo, ili mswaki ufike sehemu ambapo meno na ufizi zinakutanika mahali ambako chembechembe za chakula hujificha.Sugua sehemu zote za meno, sehemu ya nje, sehemu ya kutafunia chakula na 

sehemu ya ndani ya meno.Tumia sehemu ya juu ya mswaki kusafisha sehemu ya ndani ya meno ya juu, kwa mwendo wa juu na chini.Sugua ulimi wako kwa upole ili kuondoa vijidudu au viini vinavyosababisha harufu mbaya.Sukutua na hifadhi mswaki wako sehemu nzuri na salama kwa matumizi ya baadaye.

No comments

Powered by Blogger.