Majaliwa awapa siri wachimbaji wa madini, awatoa hofu kuhusu mikopo
“Msihofu kukopa, kukopa ni jambo la kawaida sana. Nendeni mkakope ili mpate mitaji ya kununua mitambo ya kuchenjua dhahabu na madini mengine,” amesema.
Ametoa wito leo (Jumapili, Septemba 30, 2018) wakati akifunga maonesho ya mkoa wa Geita ya dhahabu, madini, teknolojia ya madni na uwekezaji yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita. Maonesho hayo yalianza Septemba 24, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema, wakati akikagua mabanda ya maonesho kwenye viwanja hivyo, ameelezwa kwamba gharama ya mtambo unaohitajika kwa wachimbaji wa kati inafikia sh. milioni 10. “Naomba niwaeleze wana Geita kwamba mnakopesheka, nendeni mkaombe mikopo ili mnunue mitambo ya kuchenjua dhahabu,” amesisitiza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaeleza wana-Geita kwamba siri kubwa ya kufanikiwa kupata mikopo ni kwa wao kuunganisha nguvu kwa kujiunga kwenye vikundi ili wawe na malighafi ya kutosha mitambo hiyo.
“Wakuu wa wilaya za Mkoa huu simamieni zoezi hili kwa sababu wilaya zenu zote zinachimba madini. Simamieni uundaji wa vikundi na mwende mkawasemee benki pale wanapokwama.”
Akielezea kuhusu makusanyo ya fedha kutokana na mauzo ya dhahabu kwenye mkoa huo, Waziri Mkuu amesema tangu Aprili mwaka huu, mapato yanayotokana na madini yameongezeka kutoka sh. milioni 400 na kufikia sh. milioni 850 Agosti, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wazazi wawapeleke watoto wao kwenye vyuo vya ufundi vya VETA ili wakajifunze taaluma ya uchongaji wa madini na vito kama eneo jipya la ajira nchini.
“Nimemuona binti mmojakwenye banda la VETA akielezea vizuri kuhusu uchongaji wa madini na vito. Nikabaini kumbe jambo hili linaweza kufanyika hapa nchini kwetu. Ninawasihi Wazazi pelekeni watoto wenu kwenye vyuo vya VETA vya Mwanza, Geita na Moshi ambako kozi hii inafundishwa,” amesisitiza.
Post a Comment