Zijue faida zitokanazo na kusikiliza mziki kiafya

 

Kama unapenda kusikiliza mziki basi uko kwenye kundi zuri. Watu mbalimbali maarufu wamewahi kutoa maoni yao kuhusu mziki kama vile mwanabayolojia Charles Darwin aliyesema kuwa angepewa nafasi ya kuIshi tena angetengeneza kanuni ya kusoma mashairi na kusikiliza mziki angalau mara moja kwa wiki. Kwa upande mwingine Albert Einstein alikiri kuwa asingekuwa mwanafizikia basi angekuwa mwanamziki.

Tafiti zinabainisha kuwa kusikiliza mziki kuna manufaa mengi kwa ajili ya afya ya mwili na akili. Tafadhali fuatana nami katika makala hii ili nikujuze faida  za kusikiliza mziki.

Mziki hutufanya tuwe na furaha
William James alsisema “Siimbi kwa sababu ninafuraha, bali nafurahi kwa kuwa ninaimba” .

Kusikiliza mziki huzalisha kemikali ya dopamane ambayo hutufanya tujisikie vizuri. Hii ndiyo sababu mtu akiwa anajisikia vibaya au kukosa furaha mara nyingi anaposikiliza mziki hasa wa taratibu hujisikia vizuri.

Hivyo basi, wakati ukiwa umekosa raha unaweza kusikiliza nyimbo unazozipenda angalau kwa dakika 15 ili kukuweka katika hali nzuri zaidi.

Huongeza ufanisi katika kukimbia
Mtafiti Marcelo Bigliassi  na wenzake walibaini kuwa wakimbiaji wanaosikiliza mziki walimaliza mbio za mita 800 haraka zaidi kuliko wengine. Hivyo ni dhahiri kuwa kusikiliza mziki wakati wa kukimbia kunaweza kuwa kama hamasa zaidi. Unaweza kusikiliza mziki wa haraka haraka au taratibu kulingana na vile unavyopendelea.

Mziki huondoa msongo na kuboresha afya
Kusikiliza mziki hupunguza kwa asilimia 60 homoni zinazosababisha msongo (stress). Ikiwa basi msongo utapungua ni dhahiri kuwa pia maradhi mengi ambayo chanzo chake ni msongo yatapungua kama si kwisha kabisa. Unaweza kusikiliza mziki na kuimba wakati mziki unapoimba; pia usisahau kucheza angalau kwa kuchezesha mguu ili kupata tiba hii kamili.

Hukuwezesha kulala vizuri
Kusikiliza mziki husafisha ubongo wako na kuuweka katika hali nzuri itakayokuwezesha kupata usingizi mzuri.

Ulishawahi kujiuliza ni kwanini ukisikiliza mziki wa taratibu mara nyingi unapatwa na usingizi? Ni dhahiri kuwa mziki una nafasi kubwa katika kulala kwetu. Inashauriwa wakati wa usiku kuweka ubongo wako katika hali nzuri ili uweze kulala vyema; unaweza kusikiliza mziki wa taratibu kabla ya kulala.

Mziki hukuweka katika hali nzuri unapoendesha gari
Wakati mwingine kuendesha gari ni kazi inayochosha; hivyo inahitaji kiburudisho ili kuifanya vyema. Ni dhahiri kuwa madereva wanaoendesha magari masafa marefu hupenda kusikiliza mziki ili kujiweka katika hali (mood) nzuri. Hivyo basi, unaweza kusikiliza mziki unapoendesha gari. Kumbuka kuzingatia sheria za barabarani; usisikilize kwa sauti kali kiasi cha kushindwa kusikia sauti nyingine barabarani kama vile honi ili kuepuka ajali.

Hukuwezesha kujifunza na kukumbuka
Baadhi ya watu wamebainisha kuwa wanaposoma au kujifunza mambo kadhaa wakati wakisikiliza mziki, basi hufanikiwa kuyamudu maswala hayo vyema. Si jambo la kustaajabisha kuwaona watu wakisikiliza mziki huku wakisoma vitabu, majarida, tovuti nk. Hata hivyo, hili linategemea mtu na mtu, wengine hawapendi kusoma au kujifunza huku wakisikiliza mziki, wakati wengine hupenda kufanya hivyo. Hivyo uamuzi ni wako kuwa unapenda mziki au laa; na ni mziki wa namna gani unaopenda wakati wa kusoma na kujifunza.

Hupunguza maumivu
Mwanamziki Bob Marley alisema “Jambo zuri kuhusu mziki ni kuwa unapokupiga hausikii maumivu”

Pia utafiti uliofanyika katika chuo cha Drexel cha Philadelphia ulibaini kuwa mziki wa taratibu au wa jadi, hupunguza maumivu kwa wagonjwa wa saratani pamoja na wale walioko katika kitengo cha uangalizi maalumu (ICU). Je bado hauhitaji kusikiliza mziki? Naamini sasa unahitaji.

Hukuhamasisha
Wakati mwingine unakata tamaa au unakutana na mawimbi mengi sana maishani kiasi cha kuzidiwa. Ni dhahiri ipo miziki inayotia watu moyo na kuwahamasisha. Ipo mifano ya watu wengi waliotaka kujiua lakini baada ya kusikiliza miziki inayowaeleza umuhimu wa kuendelea mbele na maisha walisitisha mpango wao. Hivyo kusikiliza mziki kunaweza kukuhamasisha kuendelea kutoka ngazi moja hadi nyingine.

Hukukumbusha mambo
Ni dhahiri kuwa miziki mingi huambatana na matukio au vipindi fulani vya muda. Si jambo la kustajabisha ukasikia mziki fulani ukakukumbusha matukio au eneo fulani ulilokuwa zamani. Watu wamekuwa wakikumbushwa matukio ya furaha kama vile ndoa, mahafali, au hata ya uzuni kama vile misiba na maradhi. Hivyo ni wazi kuwa kwa njia ya mziki tunaweza kukumbuka matukio au watu fulani tuliowahi kukutana nao maishani mwetu.

Ni dhahiri kuwa yapo manufaa kadha wa kadha yatokanayo na kusikiliza mziki. Ni wazi kuwa mziki huboresha na kuweka afya za miili na akili zetu katika hali nzuri. Kama mziki una tija hivi kwa nini husikilizi ili nawe unufaike? Chagua mziki unaoupenda na uanze kusikiliza ili  nawe unufaike. Kumbuka! Sikiliza mziki kistarabu na kwa kiasi; hakuna haja ya kufungua mziki kwa sauti ya juu mtaa mzima au kusikiliza mziki saa 24 bila kufanya kazi kwa kigezo tu kuwa kuna manufaa

No comments

Powered by Blogger.