Mbinu itakayokusaidia kuongeza uwezo wako wa kufikiri
Habari za muda huu Mpenzi msomaji wa Muungwana Blog, naomba nikualike ili tuweze kujifunza mbinu ambayo itatusaidia kufikiri vyema.
Niliwahi kuandika katika maandiko yangu kipindi cha nyuma nikisema hapa duniani hakuna kazi ngumu kama kazi ya kufikiri, kama ukiweza kufikiri vyema ndiyo siku pekee utayokuwa umeushinda ule mtihani wa ugumu wa maisha, nasema hivi kwa sababu miongoni mwa uvivu ambao unayatawala maisha ya wengi ni pamoja na uvivu wa kufikiri pamoja na uvivu wa kutenda.
Leo nitakujuza japo kwa uchache kuhusu uvivu wa kufikiri ambapo nitakueleza ni kwa jinsi gani unavyoweza kuondokana na uvivu wa kufikiri hatimaye kujipatia mafanikio unayoyatarajia.
Kama ambavyo huwa unatenga muda kwa ajili ya kula, kulala, kunywa, kusoma na mambo mengine kama hayo vivyo hivyo unatakiwa kutenga muda huo huo kwa ajili ya kufikiri mambo yako ya msingi.
Wakati unapotenga muda huu wa kufikiri hakikisha unafunga pingu za maisha, ili kuhakikisha hauvunji nadhiri juu ya muda huo uliotenga kwa ajili ya kufikiri. Na katika kufanya hivyo hakikisha unawekeza akili yako katika hali ya utulivu, pia hakikisha unakaa mbali na vitu vitakavyokufanya usiweze kufikiri vizuri, vitu hivyo ni kama Runinga, Simu au kelele zozote.
Kwani ukikaa karibu na vitu ambavyo vinasabaibisha usiweze kufikiri vyema utashindwa kufaulu mtihani wa kufikiri vyema mambo yako ya msingi.
Mwisho nimalize kwa kusema ya kwamba unapofikiri unatakiwa kuchagua kitu kimoja cha kufikiri, fikiri juu ya kitu hicho mpaka upate majibu sahihi moja kwa moja katika utekelezaji wa jambo hilo.

Post a Comment