Maalim Seif na ndoto yake ya Urais 2020 itatimia akiwa na Chadema?



Baraza la Wazee la Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema limebainisha mipango ya kumshawishi Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) 

na Makamu wa kwanza wa zamani wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (2010-2015), Maalim Seif Sharrif Hamad kuwa mgombea wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 visiwani Zanzibar. 

Tamko la Wazee wa Chadema lililotolewa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Hashimu Issa Juma, limekuja katika kipindi ambacho chama cha CUF kimekumbwa na mgogoro wa uongozi tangu mwaka 2015. 

Hii ni baada ya aliyekuwa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wake kuelekea uchaguzi mkuu kisha mwaka 2017 kurejea kwenye cheo hicho kinyemela licha ya kueleza kuwa baadhi ya wanachama wamemuomba arudi madarakani. 

Kurudi kwa Lipumba ndani ya Cuf kumetengeneza makundi mawili. Kundi la wanaomuunga mkono Profesa huyo na jingine likiwa upande wa Maalim Seif. 

Mvutano unaosababishwa na makundi hayo unaonekana kuwa mkubwa. Kuna dalili kkwamba huenda ulichangia baadhi ya viongozi akiwemo Julius Mtatiro akikihama chama hicho pamoja na wabunge wa viti maalumu waliomuunga mkono Maalim Seif kupoteza ubunge wao. 

Nia ya baraza la wazee wa Chadema imetafsiriwa kuwa mbinu ya kuongeza ushawishi wao katika siasa za Visiwani Zanzibar kwa kuwa chama hicho hakina nguvu za kutosha wala kuwa na mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa visiwani humo. 

Maalim Seif mwenye miaka 74 alizaliwa Oktoba 22, 1943 kisiwani Pemba na jina lake halisi ni Seif Sharif Hamad. Maisha na shughuli zake ndizo zilichangia aitwe Maalim Seif kwa kuwa alikuwa miongoni mwa watu wanaojihusisha na jamii moja kwa moja. 

Swali moja linalotakiwa kujibiwa, Maalim Seif amefika tamati au ni mwanzo wa kutikisa tena siasa za Zanzibar? 

Maalim Seif ni miongoni mwa wanasiasa ambao wanasifika kwa misimamo pamoja na mikakati ya kisiasa. 

Ni miongoni mwa wanasiasa wanaopendwa visiwani Zanzibar. Tangu akiwa mwanachama wa CCM alikuwa mmoja wa makada wenye ushawishi ndani ya chama visiwani Zanzibar. 

Akiwa CCM amewahi kuwa Mjumbe Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Waziri wa Elimu wa visiwa hivyo kati ya mwaka 1977-1980. 

Maalim Seif alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kati ya mwaka 1980-1989, pia Mbunge wa Jamhuri ya Tanzania mwaka 1977. 

Aidha, alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kati ya mwaka 1977 hadi 1987 pamoja na kuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango wa CCM kati ya mwaka 1982 hadi 1978. Baadaye alikuwa waziri kiongozi wa Zanzibar kuanzia Februari 6, 1984 hadi Januari 22, 1988. 

Hata hivyo mwaka 1988 ulikuwa wa mwisho kwake CCM, baada ya kufukuzwa kutokana na mgogoro wake na maofisa wa chama hicho. 

Miongoni mwa rekodi ya kukumbukwa ni kwamba jina la Maalim Seif linaleta sura nyingine ya mgongano mkubwa wa maslahi ndani ya CCM Zanzibar, kati yake na aliyekuwa Rais wa visiwa hivyo Aboud Jumbe. 

Taarifa mbalimbali zinamtaja kuwa Maalim Seif ndiye mwanasiasa aliyemdokezea Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuhusu azima ya Rais Jumbe kuhoji muundo wa muungano wa Tanzania. 

Rais Jumbe pia alichukua uamuzi wa kumfukuza kazi Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Damiani Lubuva na badala yake akataka kumwajiri mwanasheria kutoka Ghana. 

Pamoja na kufukuzwa na CCM, bado Maalim Seif alionekana kubaki na nguvu zake za kisiasa hali ambayo iliwasumbua makada wengi wa chama tawala huko Zanzibar. 

Haikutegemewa kuwa Seif angepaa kisiasa licha ya kutangazwa si mwanachama wa CCM. 

Ikumbukwe wakati akifukuzwa kulikuwa na mfumo wa chama kimoja. 

Hivyo basi baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Maalim Seif alikuwa miongoni mwa wanachama walioanzisha chama cha wananchi (CUF) mnamo Mei 28, 1992 na kupata usajili wa kudumu Januari 12, 1993. 

Unaweza kutaja majina matano ya wanasiasa wenye nguvu ndani ya Chama cha CUF, ambapo Maalim Seif anakuwa miongoni mwao wakifuatiwa na mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba, Ismail Jussa Ladhu, aliyekuwa mgombea mwenza wa Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2015, Juma Duni Haji (alitokea Cuf). 

Seif ndiye katibu mkuu wa muda mrefu zaidi wa chama cha siasa nchini Tanzania. Tangu kuanzishwa chama hicho kimekuwa chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad. 

CUF ilipata usajili wa kudumu mwaka 1993 ikiwa na maana hakijawahi kupata katibu mkuu mwingine hadi hivi pale kilipokumbwa na mgogoro, ambapo upande wa Profesa Lipumba kipo chini ya ukatibu Mkuu wa Mbunge wa Kaliua mkoani Tabora, Magdalena Sakaya. 

Seif ameweka rekodi ya aina yake ambayo haijafikiwa na mwanasiasa yeyote nchini. Lakini nini sababu hasa ya Seif kubaki kuwa katibu mkuu wa muda mrefu kiasi hicho? Jawabu la swali hilo ndiyo kuibuka kwa dhana kwamba CUF ni Seif na Seif ni CUF. 

Kwamba CUF licha ya kutambulika kama chama cha siasa kinaonekana kuwa mikononi mwa Maalim Seif kuliko mwanasiasa mwingine yeyote Visiwani Zanzibar. Amepitia makatibu wasaidizi kadhaa wakiwemo Julius Mtatiro (Bara), Magdalena Sayaka (Bara), Nasoro Mazrui (Zanzibar) na wengineo. 

Je wanachama wa Cuf hawana imani na wanasiasa wengine wenye uwezo wa kuwa katibu mkuu? Kwamba Maalim Seif ndiye mwanasiasa pekee ambaye anaweza kuimudu nafasi hiyo na kukifanya CUF kuwa chama bora? Jibu ni kwamba kutokana na kuongoza kwa muda mrefu katika chama hicho amejikuta akitengeneza athari - chanya au hasi- ambayo hutoa sura ya Cuf ni Maalim Seif au Maalim Seif ni Cuf. 

Rekodi ya kugombea urais 
Rekodi nyingine iliyowekwa na Maalim Seif ni kuwa mwanasiasa aliyegombea urais mara nyingi zaidi kuliko mwanasiasa mwingine yeyote katika jamhuri ya muungano wa Tanzania. Hadi sasa amegombea urais wa Zanzibar mara 5, na iwapo mwaka 2020 atapitishwa itakuwa ni mara ya sita kuwania urais. 

Seif alianza kuisaka tiketi ya kuingia Ikulu katika uchaguzi wa mwaka 1995 kupitia chama cha Cuf ambapo alipambana na mgombea wa CCM, Salmin Amour. 

Kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) matokeo ya urais mwaka 1995, Salmin Amour alishinda kwa asilimia 50.24 dhidi ya 49.76 alizopata Maalim Seif. Hata hivyo Cuf ilitangaza kutoutambua ushindi huo. 

Mwaka 2000 Seif aliingia tena ulingoni, na safari hiyo alipambana na Amani Karume mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume. 

Kwa mara nyingine matokeo ya ZEC yalionyesha Seif aliangushwa baada ya kujikusanyia asilimia 32.96 ya kura dhidi ya asilimia 67.04 alizopata Amani Karume. 

Katika uchaguzi wa mwaka 2000 ulionyesha anguko kubwa sana la Maalim Seif kutokana na kupata asilimia chache (32.96%) tofauti na uchaguzi wa mwaka 1995. 

Tofauti hii pekee inaweza kutusaidia kutuzindua mwelekeo wa Maalim Seif kama ni mwanzo wa mtikisiko au mwisho wake kisiasa visiwani Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kwa ujumla. Hata hivyo kulikuwa na malalamiko katika uchaguzi huo ambapo baadhi ya waangalizi walisema haukukidhi vigezo vya kidemokrasia kutokana na wagombea kutoka vyama vya upinzani kutishwa na vyombo vya dola. 

Aidha, waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola walisema uchaguzi huo ulitawaliwa kwa kile walichokiita 'uchafu mwingi'. 

Vidonda vya uchaguzi wa mwaka 2000 vilijitokeza zaidi mwaka 2001 ambapo baadhi ya wafuasi wa Cuf walipoteza maisha baada ya kushambuliwa na vyombo vya dola. 

Vurugu zilizotokea Januari 27, 2001 zilichangia kusainiwa makubaliano ya pili ya amani baina ya pande mbili za Cuf na CCM ili kuleta utulivu visiwani Zanzibar. 

Uchaguzi wa mwaka 2005 ulivihusisha pia vyama vyote kinzani CCM na CUF. Kwa upande wa CUF walimsimamisha Maalim Seif na Amani Karume akateuliwa na CCM kutetea kiti chake. Mambo yaliyokubaliwa kwenye muafaka wa mwaka 2001 yalifanyiwa marekebisho kwenye uchaguzi wa mwaka 2005. 

Uchaguzi huo ulipokamilika, ZEC ilimtangaza Amani Abeid Karume kuwa mshindi baada kujikusanyia asilimia 53.18, huku Seif Hamad akijipatia asilimia 46.07. uchaguzi huo ulionyesha Maalim Seif alipanda kidogo kutoka asilimia 32.96 za mwaka 2000 hadi 46.07% za mwaka 2005. 

Hata hivyo waangalizi wa kimataifa kwa mara nyingine walisema kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki. 

Wangalizi wa Jumuiya ya Madola walisema palikuwa na kasoro nyingi na uhaba wa uhuru miongoni mwa wapigakura na wagombea. Cuf ilipinga matokeo hayo. 

Maalim Seif alirudi tena kwenye mbio za urais mwaka 2010 akiwakilisha chama cha CUF dhidi ya Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM. Baada ya uchaguzi wa Oktoba 31, 2010 ZEC ilimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar. Palikuwa na tofauti ndogo ya alama, ambapo Dk. Shein alipata asilimia 50.1 na 49.1 za Seif. 

Kutokana na makubaliano ya vyama hivyo kumaliza mgogoro wa muda mrefu visiwani humo, Maalim Seif alitakiwa kuwa sehemu ya serikali ambapo aliteuliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, huku Balozi Seif Ali Iddi akiwa makamu wa pili wa Rais. Mgawanyo huo wa madaraka ulikuwa na lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar. 

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilifuta uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, 2015 na Mwenyekiti wake Jecha Salum Jecha. ZEC ilitangaza pia uchaguzi wa marudio utafanywa Machi 20, mwaka uliofuata. 

Licha ya kufutwa uchaguzi huo, Maalim Seif aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mnamo Oktoba, 2015 na kusema yeye ndiye mshindi wa kiti cha urais Zanzibar. 

Oktoba 26, mwaka huo Maalim aliviambia vyombo vya habari, "Baada ya kukusanya matokeo yote, nimepata kura 200,007 dhidi ya kura 178,363 za mgombea wa CCM anayetetea nafasi yake, Dk. Ali Mohammed Shein." 

Mosi, mara baada ya uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2015 Maalim Seif alifanya mazungumzo na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi nchini Davies Mwamunyange. 

Pili, Seif alifanya mazungumzo na rais mstaafu Jakaya Kikwete kabla hajaondoka madarakani. Tatu, Seif alifanya mazungumzo na Dk. Shein. Nne, Seif alifanya mazungumzo na Rais John Magufuli. Mazungumzo yote hayo yalikuwa na lengo la kuleta utulivu visiwani Zanzibar. 

Raia hawakuwawahi kuambiwa hadharani mazungumzo hayo yalikuwa na makubaliano ya gani hadi leo zaidi ya 'hisia za wananchi' zilizotamalaki ingawa ajenda kuu ilikuwa ni kuhusu ni 'hali ya Zanzibar'. 

Jambo la tano ni uamuzi wa CUF kukataa kushiriki uchaguzi wa marudio na kufuta ndoto zake za kuchukua madaraka ya urais. 

Naam, sasa limeibuka suala la kuombwa kujiunga na Chadema, ikiwa na maana kuwa wafuasi wa Chadema na Cuf wanaweza kuungana na kutengeneza nguvu kubwa ya kisiasa visiwani humo na kuwa na mshikamano madhubuti. 

Akawania tena, kuna uwezekano wake kushinda? 


Atajenga umaarufu wa Chadema visiwani? 
Juhudi za Malim Seif katika siasa za Zanzibar si za kubeza hata kidogo. Ni mwanasiasa ambaye ana wafuasi wengi kila kona ya Zanzibar. Hili linafahamika vyema mbele ya wazee, viongozi na wanachama wa Chadema. 

Pia Chadema bila shaka wanatamani tena kupata uhondo wa nguvu waliopata kwenye uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 pale Juma Duni Haji alipohamia chama hicho na kuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa. 

Ile nguvu ya wafausi wa Cuf inahitajika mno Chadema, hivyo suluhisho ni kumsajili Maalim Seif. Hii ina maana kuwa iwapo Maalim Seif atakihama Cuf, wimbi la wanachama na wafuasi wake watamiminika Chadema. 

Ngome ya Maalim Seif huko Kisiwani Pemba itahamia Chadema. Hata hivyo wasiwasi unakuja kutokana na misimamo thabiti ya wafuasi wengi wa Cuf haifahamiki kama wote wataunga mkono mpango wa kwenda Chadema. 

Aidha, ukitazama kwa makini mpango wa kuhamia Chadema unaweza kutumika kama mbinu nyingine ya kumjenga Maalim Seif na kupima kuhitajika kwake ndani ya Cuf na siasa za Tanzania kwa ujumla wake. 

Pamoja na mambo yote, Maalim Seif bado ni lulu katika ulingo wa kisiasa Zanzibar na Jamhuri ya Tanzania kwa ujumla. Nguvu, umahiri na ushawishi wake vyote vinahitajika kuwa chachu ya kuwaelimisha vijana juu ya siasa za upinzani pamoja na uongozi wa taasisi na nchi. 

No comments

Powered by Blogger.