Jinsi ya kujihakikishia hewa safi ndani ya nyumba
WAKATI mwingine ukiingia nyumbani kwako kichwa kinaanza kukusumbua kwa sababu ya hewa nzito. Inatokea pia umegundua kuwa kuna harufu ambayo huifurahii ndani ya nyumba. Huenda ni vigumu hali hiyo kuimaliza.
Kuanzia hapo zinahitajika jitihada ili kuboresha hewa ya ndani ya nyumba.
Watoto na watu wenye mzio wanaweza kuhisi mabadiliko ya hewa ndani ya nyumba hata yakiwa ni kwa kiasi kidogo.
Hewa mbaya ndani ya nyumba yanaweza kuwasababishia wanafamilia matatizo ya kiafya endapo tatizo hilo halitapata ufumbuzi mapema.
Inawezekana mwanzoni likaonekana ni jambo gumu la kufanya, ila cha kuzingatia ni kwamba kusafisha hali ya hewa ya ndani ya nyumba tunazoishi ni rahisi sana.
Unachotakiwa ni kuzingatia kuwa unachoshughulika nacho ni njia zinazopitisha hewa kutoka nje na zile zinazochafua hewa. Ukifahamu njia hizo na kufahamu namna ya kuongeza ubora wa hewa ya ndani umemaliza tatizo hilo.
Wakati hewa, inapoanza kuwa nzito na huku kukiwa hakuna uingizaji wa hewa safi ndipo na vichafua hewa ndani ya nyumba vinapoanza kujijenga.
Na changamoto kubwa ya nyumba za kisasa ni kuwa zimezibwa kila mahali na ni kawaida kukuta milango na madirisha yamefungwa kwa muda mrefu kuliko yanavyofunguliwa. Njia rahisi ya kuondoa tatizo hili ni kufungua madirisha kila siku na pia kuwasha feni.
Jambo lingine ni kuzingatia usafi wa jumla, kwamba sakafu ziwe safi na zisafishwe kila inapobidi. Unapoacha taka, nguo chafu, vumbi na uchafu mwingine kujijenga unakaribisha uwezekano wa nyumba kuwa na harufu mbaya ndani ya vyumba na jikoni.
Usiruhusu vyombo vichafu vijazane kwa muda mrefu bila kusafishwa, na pia usihifadhi nguo chafu zinazonuka jasho kwa muda mrefu bila kufuliwa. Futa vumbi kila wakati.
Kama una viyoyozi hakikisha vinasafishwa mara kwa mara ili vichujo vyake visibebe vumbi na kuziba lakini pia vikisambaza mavumbi ndani. Safisha feni na tumia marashi ya kupuliza ndani ya nyumba pale inapobidi ili kupata hewa freshi.
Epuka kuwa na vifaa vyenye harufu mbaya kwa mfano kuna samani zenye gundi zinazotoa harufu kipindi chote. Ondoa mara moja dawa zenye harufu mbaya kama za mchwa, Ukiua panya usijisahau na kuacha mizoga yake kusababisha harufu mbaya.
Zipo harufu zinazotokana na wadudu kama mende kuzaliana kwenye kabati na ukutani waondoe.
Kuna harufu zinazotokana na dawa, manukato yatumikayo kwenye dawa za kusafishia. Na pia kuna harufu zinaingizwa ndani ya nyumba kupitia fenicha mpya, magodoro, mazulia au hata rangi ya ukutani. Fungua madirisha na milango ili kumaliza harufu hiyo.
Uvutaji wa sigara ndani si jambo jema. Unasababisha nyumba kunuka moshi wa sigara. Inaweza kuwa ni kero kwa mvutaji kama ndiye mwenye nyumba lakini hakuna jinsi itabidi kuacha kuvuta ndani kwa kuwa anaathiri hewa ya nyumba na kuwakera wanaoishi humo.

Post a Comment