Azam yathibitisha kumkosa mchezaji wake miezi saba
Klabu ya soka ya Azam FC imethibitisha kuwa mlinzi wake Mghana Daniel Amoah, ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti kwenye Hospitali ya Vicent Palloti jijini Cape Town, Afrika Kusini atakaa nje kwa muda wa miezi saba.
Kwa mujibu wa taarifa ya timu hiyo kuhusu hali ya nyota huyo ambaye aliumia kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la shirikisho nchini dhidi ya Mtibwa Sugar, imeeleza kuwa nyota huyo anaendelea na tiba chini ya uangalizi wa daktari wa timu.
Aidha Azam pia wameweka wazi kuwa Amoah tayari amerejea nchini Jumanne mchana baada ya upasuaji huo na anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda wa miezi saba kutoka hivi sasa kwaajili ya kupata matibabu pamoja na kuanza mazoezi mepesi.
Kwa upande mwingine kikosi cha Azam FC leo asubuhi kimefanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo wake wa ligi kuu raundi ya 24 dhidi ya RuvuShooting, utakaofanyika kesho Alhamisi Kwenye uwanja wa Mabatini Mkoani Pwani.
Post a Comment